WADAIWA KUINGIZIWA CHUPA NA RUNGU SEHEMU ZAO ZA SIRI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, kimesema watuhumiwa watano waliokamatwa na polisi wilayani Ngorongoro waliteswa, kupigwa na kuingiziwa chupa sehemu za siri. 

Aidha, watu hao waliteswa kwa madai ya kuiba mali za watalii kwenye kampuni ya Simba B, ambayo baadhi wanafanyia kazi na walikaa kwenye kituo cha polisi kwa siku 15.

Watuhumiwa hao ambao walirekodiwa kwa video wakieleza yaliyowakuta na kuonyeshwa mbele ya waandishi wa habari ni Peter Orkery, Musa Yahya, Kayanda Kisoki, Zakaria na Francis Arusha.

Kutokana na hali hiyo, wanaharakati hao wametangaza kuanzisha mpango wa kuwasaidia watuhumiwa wote wanaoteseka kwenye vituo vya polisi, kupaza sauti kupitia mitandao ya kijamii, ili kuwashinikiza polisi kuacha unyanyasaji wa raia.

Wakizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, Ofisa Programu wa LHRC, Paulo Mikongoti na Mtafiti wa LHRC, Tito Magoti, walisema matukio ya watu kuteswa, kujeruhiwa, kuuawa na kunyimwa haki zao wakiwa mikononi mwa polisi, yanaongezeka kila siku nchini.

“Tukichukua mfano wa tukio la Loliondo awali watu sita waliteswa na walikaa kituoni kwa zaidi ya siku saba na kuachiwa bila kufunguliwa kesi. Sasa kuna watu watano nao wamekaa vituo tofauti vya polisi kwa siku 15 na hawajafikishwa mahakamani na sasa wanauguza majeraha makubwa yaliyogharimu afya zao,” alisema Mikongoti.

Alisema walipokamatwa na polisi walichukuliwa kwa ajili ya kutoa maelezo walipofika kituoni walifungwa kamba mikononi na miguuni kisha wakatundikwa juu na kuanza kupigwa hadi miguu kupasuka.

“Baada ya mahojiano watuhumiwa walidai kufanyiwa ukatili wa kutisha kwa kuingiziwa rungu za polisi na chupa sehemu za haja kubwa na kutakiwa kunusa. Hali zao ni mbaya na wengine bado wanauguza majeraha yaliyotokana na vipigo na ukatili waliofanyiwa na askari wa polisi kituo cha Loliondo,” alisema Mikongoti.

Alisema baada ya kukamatwa Desemba 21, mwaka jana na kukaa mahabusu kwa siku 15 bila kuonana na ndugu zao, miguu ya baadhi ya watuhumiwa ilianza kuoza wakapelekwa mahakamani Januari 4, baadaye walilazwa hospitali ya Wasso kwa ajili ya matibabu na walifanyiwa upasuaji kwenye miguu na kutolewa usaha uliokuwapo kwenye miguu.

Via Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post