MMILIKI WA SHULE MATATANI KWA KUWATWANGA RISASI WALIMU ARUSHA

Picha
JESHI la Polisi mkoani Arusha limemsweka ndani mmiliki wa shule binafsi ya Usa Academy iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha, Robert Lukumay, maarufu kwa jina la Naibala, kwa tuhuma ya kuwajeruhi kwa kuwapiga risasi walimu wawili wa shule hiyo, baada ya walimu hao kudai malimbikizo ya mishahara yao.


Mbali ya kuswekwa ndani kwa kosa la kujeruhi, pia silaha tatu za mmiliki huyo zinashikiliwa na polisi, ikiwemo bastola ili kuchunguza kama anamiliki kihalali.

Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Ng'azi alithibitisha kushikiliwa kwa Nabalala na aliwataja walimu walijeruhiwa na wako hospitali kwa matibabu kuwa ni Pretus Richard na Annet Mollel.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Jerry Muro amesema, Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo yeye ni Mwenyekiti wake, iliagiza kukamatwa kwa Naibala kwa uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo na yuko ndani hadi jana.

Muro alisema mbali ya hilo, kamati hiyo ilikwenda mbali zaidi na kumfanyia upekuzi nyumbani kwake na kukuta silaha tatu, ikiwemo shotgun, rifle na bastola.

Alisema kamati ilipofika katika geti la shule hiyo, ilikuta kufuli la geti limepigwa risasi na maganda ya silaha yakiwa chini na walipochunguza, waligundua kuwa maganda hayo ni ya silaha aina ya shotgun, ambayo ndiyo ilikuwa ya mmiliki wa shule hiyo.

Muro alisema hatua ya kwanza aliyochukua yeye kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, ni pamoja na kuchukua silaha zake zote, lengo ni kutaka kujiridhisha kama kweli anamiliki kihalali silaha hizo.

Alisema kingine kilichodunguliwa kwa mmiliki huyo ni dalili za awali, kuonesha kuwa silaha aina shotgun ilitumika katika tukio hilo.

Muro alisema kutoka na hali hiyo, aliunda kamati ya watu wachache kuchunguza tukio hilo la silaha hizo tatu, kama ni mali ya mmiliki huyo na kuchunguza tukio zima la walimu kujeruhiwa kwa risasi na kazi hiyo ifanywe ndani ya wiki moja. “Hili ni suala zito sana, hatuwezi kuona wamiliki wa shule wanafanya vitu vya hovyo hovyo namna hii hasa hivi vya kupiga risasi walimu wakati wakidai haki yao ya msingi, hilo halitavumiliwa,” alisema Muro.

Walimu waliojeruhi walisema kuwa wanadai mishahara ya miezi sita katika shule hiyo na wanapomfuata mmiliki wa shule hiyo, majibu yake ni ubabe na vitisho, bila ya sababu za msingi.

Mwalimu Mollel alisema katika shule hiyo, wako walimu 27 na wote wanadai stahiki zao mbalimbali, ikiwemo mishahara ya miezi sita na wamekuwa wakifanya kila jitihada kupata haki hiyo katika ngazi mbalimbali bila ya mafanikio.

Kamanda Ng'azi alisema Polisi inamshikilia Nabalala kwa uchunguzi zaidi; na akibainika ana makosa, atafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu mashitaka.

Alisema kwa sasa Naibala yuko rumande katika Kituo cha Polisi Usa River kwa upelelezi ;na uchunguzi ukikamilika, polisi itatoa taarifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527