RC AINGILIA KATI SAKATA LA MKURUGENZI KUPIGANA MAKONDE NA OFISA USALAMA WA TAIFA WA WILAYA (DSO)


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, ameingilia kati sakata la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva, kudaiwa kupigana makonde na Ofisa Usalama wa Taifa wa Wilaya (DSO), Abdi Musa.

Mghwira amesema ametuma timu ya maofisa mbalimbali kwenda kuwahoji maofisa hao ili kujua chanzo chake na hatua za kuchukua.

Kuchapana makonde kwa maofisa hao kumetokea zikiwa zimepita siku 24 tangu Mawaziri Selemani Jafo (Ofisi ya Rais, tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi) na Kapteni (mstaafu) George Mkuchika wa pia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupiga kambi mkoani Kilimanjaro kutafuta suluhu ya uhusiano wa kutia shaka baina ya wateule  hao wa Rais.

Viongozi hao wanadaiwa kupigana juzi  mchana ikiwa ni saa chache tangu Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho, adaiwe kutoa amri ya kuwekwa ndani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa kabla ya tukio hilo, asubuhi kulikuwa na kikao katika ukumbi wa halmashauri ambacho mkurugenzi alipaswa kuhudhuria lakini hakutokea, hivyo kutuma mwakilishi.

Inadaiwa kuwa uamuzi wake wa kutuma mwakilishi, hakumpendeza ofisa usalama huyo na kuamua kumfuata ofisini kwake.

Baada ya kufika, inaelezwa kulitokea kutoelewana na ndipo wakashikana mashati na kuanza kutwangana makonde.

Alipotafutwa kuzungumzi tukio hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo (Mbogho) alisema hana taarifa lakini akaomba apewe muda wa kufuatilia kujua usahihi wa taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Lubuva alipoulizwa kuhusiana na taarifa za kuhitilafiana na ofisa huyo na kisha kupigana, alisema anaiachia mamlaka husika ifanye kazi yake.


Chanzo - MPEKUZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post