SIMBA YATAJA MASHARTI YA MKATABA WA KOCHA AUSSEMS


Kocha Patrick Aussems

Kufuatia gumzo kubwa mitandaoni baada ya Simba kutolewa katika mashindano ya SportPesa, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi juu ya makubaliano ya mkataba wa kocha mkuu, Patrick Aussems.

Hatua hiyo imefikia baada ya mashabiki wengi wa Simba kukasirishwa na kitendo cha klabu hiyo kushindwa kusonga mbele katika mashindano hayo, ikitolewa na Bandari FC ya Kenya.

Akizungumzia juu ya matokeo yasiyoridhisha na hatma ya kocha Aussems, Ofisa Habari wa Simba , Haji Manara amesema katika mkataba wa Simba na kocha huyo hakuna makubaliano juu ya makombe mengine zaidi ya kombe moja na sharti ambalo tayari amelitimiza.

"Kwenye mkataba wa Aussems tumemwambia kwamba tunahitaji atufikishe hatua ya makundi ya Klabu Bngwa Afrika jambo ambalo amefanikiwa kulifanya na lipo kwenye mkataba pamoja na kutupatia ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao upo mikononi mwetu", amesema Manara.

"Hayo makombe mengine hatujaweka kwenye makubaliano tunashiriki kulinda heshima na tukifanikiwa kupata ni jambo jema hivyo kushindwa kuyapata kwetu haina maana kwamba kocha hafai hapana tuna mipango yetu na tunafanya kazi kwa utaratibu", ameongeza.

Katika siku za hivi karibuni, Simba imeshuhudia ikipoteza nafasi moja ya kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kuondolewa na Mashujaa FC katika mzunguko wa nne wa kombe la shirikisho, ambapo hivi sasa inategemea nafasi ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara au ishinde ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika ili ipate tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post