MITIHANI KIDATO CHA PILI ILIYOFUTWA KUFANYIKA JAN 14 - 22


Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema mitihani ya kidato cha pili iliyofutwa mwishoni mwa mwaka jana, sasa itafanyika tena wiki ijayo katika shule zote za Unguja na Pemba.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali anayeshughulikia Taaluma, Madina Mjaka Mwinyi alisema mitihani hiyo itafanyika Januari 14 hadi 22 kwa wanafunzi wa shule za Serikali na binafsi.

 Aliwataka walimu wakuu wote kukamilisha maandalizi ya mitihani hiyo ili kuhakikisha hakuna dosari zinazoweza kujitokeza. 

“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inatangaza rasmi kwamba mitihani ya kidato cha pili iliyofutwa Desemba 3 mwaka jana itafanyika tena wiki ijayo tarehe 14 hadi 22 nchini kote” alisema.

Akifafanua, alisema mitihani hiyo imetungwa tena baada ya kufanyika kwa udanganyifu mkubwa na kusababisha wizara kufuta mitihani ya awali. Mjaka aliwakumbusha wasimamizi wa mitihani hiyo, kufuata maadili na kanuni za mitihani, ikiwemo kuepuka aina zote za udanganyifu. 

Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu mtendaji atakayebainika kujishughulisha na udanganyifu, ikiwemo kumsaidia mwanafunzi kupata majibu ya mitihani.

“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inawataka wasimamizi wa mitihani kuhakikisha kwamba wanafuata maadili na kanuni za masharti ya mitihani ikiwemo kuepuka udanganyifu,” alisema. 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juman (pichani) aliitangaza rasmi kufutwa kwa mitihani ya kidato cha pili, siku moja baada ya wanafunzi kuanza mitihani hiyo kutokana na kuvuja kwa mitihani hiyo na matokeo yake.

SOMA PIA

Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa ya Kidato cha Pili (FTNA) 2018 Na Darasa la nne (SFNA) 2018 yametangazwa..Yaangalie hapa na pia mpangilio wa ufaulu ngazi ya mikoa na halmashauri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post