FUGA MENDE UTAJIRIKE

Na Joseph Sabinus

Mende ni mdudu anayechukiwa na watu wengi katika jamii kwa kuwa anahusishwa na uchafu sambamba na kusambaa kwa maradhi mbalimbali licha ya wadudu hawa kuwa na manufaa makubwa kwa binadamu ambayo hayajajulikana kwa wengi.


Lucius Kawogo ni mkazi wa wilayani Njombe akijishughulisha na ujasiriamali wa namna tofauti ukiwemo wa kufuga samaki, kuku, sungura, nyuki na pia, anafuga mende kwa ajili ya chakula cha samaki na kuku anaowafuga sambamba na mende kwa ajili ya biashara (kuuza).

Kawogo anayefanyia ufugaji wake wa mende katika Kijiji cha Igawisega, Kata ya Wino wilayani Madaba mkoani Njombe, anasema japo amefanya shughuli hiyo kwa takribani miezi sita iliyopita, anaona ufugaji wa mende ni kazi ndogo na rahisi, lakini yenye faida.

“Nimeanza kuongeza uzalishaji wa kuku na samaki kwa kufuga mende kwa ajili ya chakula cha mifugo hao kwa kuzingatia lishe na matunzo ya wadudu hao ambao bado kwa watu wengi hawafamu kuwa ni chakula kizuri… Mende wana kiasi kikubwa sana cha protini.” anasema.

“Kwa kweli, watu hawajajua tu, lakini ufugaji wa mende ni biashara inayolipa sana na ndiyo maana ninatamani wengi waifanye kazi hii ili hata ninapokuwa na oda nyingi kiasi cha mimi kupungukiwa, wateja wangu wasikose mzigo, bali nichukue kwa wafugaji wengine na kutimiza mahitaji ya wateja wangu huku pia, nikiwa nimesaidia biashara kwa wafugaji wenzangu.”

Anapozungumza katika mafunzo kwa wajasiriamali 1,000 yaliyoandaliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) mjini Njombe hivi karibuni, Kawogo anasema anajuta kuchelewa kurasimisha miradi yake hali ambayo ingemwezesha kupata mtaji mkubwa na mapema zaidi.

“Kuchelewa kurasimisha miradi yangu kumenikosesha fursa nyingi maana siwezi hata kupata mkopo na kama ningekuwa nimerasimisha, ningepata soko na wateja wengi na ningetambulika na kujitangaza zaidi.” anasema.

“Nimewaomba Mkurabita wanisaidie kuniunganisha na benki ili benki inikopeshe mtaji wa kufanya ufugaji wangu mkubwa wa samaki, kuku, mende na vingine, lakini kwa masharti nafuu; yaani, nipewe muda wa kutosha kuanza marejesho tofauti na hali ilivyo kwa taasisi nyingi, unapewa leo mkopo, wiki hii hii unatakiwa uanze marejesho sasa unajiuliza kama sijaanza uzalishaji, hayo marejeso nitayatoa wapi, labda nikate pesa zilezile walizonipa, niwarejeshee…” anasema.

Mratibu wa Kitaifa wa Mkurabita, Seraphia Mgembe anasema: “Baada ya kumsikia akisema anatafuta namna ya kupata mkopo benki ukiwa na masharti nafuu, tuliwasiliana na kumuunganisha na benki ya CRDB, Tawi la Njombe nao wakasema, wako tayari kumsikiliza aende wazungumze.”

Meneja Urasimishaji Biashara wa Mkurabita, Harvey Kombe, anasema walipomtembelea Kawogo kuona namna anavyofanya shughuli zake hivi karibuni, walibaini maendeleo katika ufugaji wa samaki sambamba na ufugaji wa memde anaotumia kulishia samaki na kuonesha manufaa makubwa. Mintarafu mazungumzo na CRDB kuhusu mkopo huo, Kombe anasema: “Bado wapo kwenye mazungumzo…”

Kawogo amekiri kuwa katika mazungumzo hayo na CRDB. Anasema: “Bahati nzuri Mkurabita hao hao, wamenikutanisha pia na SIDO ambao wamekubali kunikopesha Sh 5,000,000 ili marejesho yaanze baada ya miezi 12….”

Mjasiriamali huyu anasema alianza na mtaji wa mende wa Sh 150,000 aliponunua boksi moja la mende wazazi 100 kutoka Kenya na sasa anafuga takriban mende 50,000 katika maboksi matano yenye takriban mende 10,000 kila moja na anakusudia kuongeza mengine.

Anasema asili ya wazo la ufugaji mende ni picha ya video aliyoona katika mitandao ya kijamii na kisha, akafuatilia na kusoma kwenye mitandao kwamba kuna uwezekano wa kufuga mende na funza ndipo akabaini uwezekano huo na manufaa yake. “… Nilikwishauza mende zaidi ya 600. Mende mmoja anauzwa kwa Sh 500 na yai moja la mende, linatoa watoto takriban 50…”.

Anabainisha kuwa, wateja wake wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Dodoma, Mwanza, Bukoba (Kagera), Mkuranga (Pwani), Dar es Salaam na Kigoma na kwamba, hajawahi kupata mteja kutoka Njombe.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam, Judica Losai anasema amevutiwa na bidhaa hiyo ya mende na kuweka oda ya mende 50 na maboksi mawili kwa mfugaji huyo ili kulishia bata anaowafuga.

Losai anasema: “Nitamshauri hata mwanangu Enoth Lyimo anayefuga pelege (samaki) na kuku huko Mlandizi (mkoani Pwani) ili naye aanzishe ufugaji wa mende kulishia samaki wake.”

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Menardy Mlyuka anampongeza Kawogo kwa ubunifu wa kufuga vitu (mende) ambavyo faida zake hazijafahamika vema kwa jamii.

Kawogo anasema ili mende wasisambae na kuwa kero kwa wakazi na maeneo jirani, huwajengea maboksi yasiyoruhusu hata mende mdogo kutoka, lakini akizingatia kuwaacha mianya ya kupitisha hewa ili wasife.

“Hapo ninapowafugia, pia kuna kuku wengi hivyo, ikitokea mende akatoroka, hawezi kufika mbali maana atagombaniwa na kuku. Unajua kuku wanapenda sana kula mende,”anasema.

MANUFAA Anapozungumzia manufaa aliyokwisha yapata katika ufugaji wa mende, Kawogo anasema:

“Mende ambao nimewauza, nimefanikiwa kutumia fedha kuchonga maboksi mengine, nimenunua sungura ninaowafuga na wengine nimekuwa nikiwatumia kukausha na kuwasaga kwa ajili ya kutengeneza chakula cha samaki na kuku ambao tangu waanze kula mende, wamekuwa na afya bora na uzalishaji mayai umeongezeka maradufu… wanataga sana”.

Anapoulizwa kama wateja au walaji wa kuku na samaki anaowafuga hawachukii wanaposikia wanakula chakula kinacholishwa kwa mende,

Kawogo anasema: “Wateja wanaposikia hivyo, wanafurahi kweli maana kwanza wanajua mende wanaprotini nyingi, na pia hawana chemikali kwa hiyo wanakula vyakula ambavyo havijalishwa kemikali. Watu hawataki kula kuku waliokuzwa kwa kulishwa kemikali…”

SOMA ZAIDI HAPA
Via Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post