Baada ya mpango wake wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kukataliwa bungeni na yeye pia kuponea kura ya kutokuwa na imani naye, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May sasa anajaribu kuwashirikisha wapinzani.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May leo anakabiliwa na mkwamo mwingine kuhusu mpango mpya wa mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya - Brexit.
Hii ni baada ya May kupata ushindi mdogo kwenye kura ya kutokuwa na imani naye, kufuatia kushindwa kwa mpango wa awali wa Brexit.
May na waliounga mkono mpango wake, walipata kura 202 pekee huku walioupinga wakipata kura 432 bungeni.
Bibi May amewatolea wito viongozi wa upinzani kukutana naye kwa mazungumzo ya pamoja ya vyama vyote vya kisiasa, kabla ya kuwasilisha pendekezo mbadala kwa bunge la nchi hiyo siku ya Jumatatu wiki ijayo.
Lakini wapinzani wake wamewasilisha orodha ya matakwa yao ili kuwezesha ushirikiano na May, ikiwemo kufuta uwezekano kwamba Uingereza itaweza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya mwezi Machi bila ya makubaliano kabisa.
Hata hivyo bibi May amesema milango bado iko wazi kwa yeyote kushiriki.
Hayo yakijiri nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zinajadiliana kuhusu namna ya kusonga mbele baada ya bunge la Uingereza kuyakataa makubaliano ya May kuhusu Brexit.
Uingereza inatarajiwa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29.
Chanzo:Bbc