MABINTI WACHAPANA MAKONDE BAADA YA JAMAA KUWAAMBIA ANAOA MREMBO MWINGINE

Picha haihusiani na habari hapa chini
Mabinti wawili wanauguza majeraha ya kuwekeana baada ya kutwangana makonde wakizozania jamaa mmoja eneo la Kithyoko Kaunti ya Machakos nchini Kenya waliyekuwa wakimmezea mate.


 Inadaiwa kwamba jamaa huyo aliwaalika kwake na kuwaarifu kuhusu mipango yake ya kutaka kuoa karibuni kwani tayari alikuwa amepata binti wa kumuoa. 

 “Mimi nimewaita hapa tukae kama marafiki, lakini cha muhimu ningependa kuwaalika rasmi kwenye harusi yangu itakayofanyika karibuni,” jamaa huyo aliwaambia. 

Katika ripoti ya Taifa Leo la Alhamisi, Januari 31 inadaiwa kuwa, kusikia maneno ya jamaa huyo, mabinti hao walianza kukunja sura zao kwa mshtuko mkubwa huku kila mmoja wao machozi yakimlengalenga. 

 “Loh! Unamaanisha nini? Una hakika unajua unachosema wewe?” Mmoja wao aliuliza kwa mshangao huku ameikunja sura.

 “Najua kila mmoja wenu alitarajia mazuri kutoka kwangu. Lakini poleni sana kwa kuwa hivi sasa nina mchumba nitakayefunga naye pingu za maisha karibuni. Sasa komeni kujipendekeza kwangu na kila mtu ajitafutie maisha yake,” jamaa alisema.

 Inadaiwa mabinti hao walishindwa kujizuia na ghafla wakaanza kutwangana mangumi huku kila mtu akimlaumu mwenzake kwa kumharibia asiolewe na jamaa huyo.

 “Ni wewe… balaa hii yote ni wewe,” mmoja wa mabinti hao alimwambia mwenzake akimwonyesha kidole.

Inaelezwa kuwa binti mwenzake alimjibu kwa maneno ya kukera huku akimkejeli mwenzake aliyekuwa amemwonyesha kidole. 

 “Chunga mdomo wako. Si ulikuwa ukiringa utaolewa naye. Umekula hu!” alisema na wote kupigana na kuangushana hadi sakafuni huku jamaa akiwatenganisha.

 “Tokeni hapa sasa mumezidi. Nimewaambia msijipendekeze kwangu tayari nina mchumba wa kuoa. Sijui mnapigania nini sasa. Hebu! Kila mtu nje mkapiganie huko,” jamaa huyo aliwavuta na kuwaondoa nje kisha akaufunga mlango wake.

 Mabinti hao walizozana nje kwa muda kabla ya kila mtu kushika hasini zake na kutokomea baada ya majirani na watu kujikusanya kuangalia sinema ya bure. 

Via Tuko 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post