Mahakama Kuu Tanzania imeipa siku saba Serikali kuwasilisha utetezi wake katika shauri la maombi ya kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, tofauti na muda uliowekwa kisheria wa siku 14.
Kesi hiyo imefunguliwa na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili, Joran Bashange na Salim Biman wa CUF kwa niaba ya muungano wa wanachama wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Uamuzi huo umetolewa leo mchana Ijumaa Januari 4, 2019 na kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo, Jaji Barke Sahel.
Ametoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na maombi ya waombaji katika shauri hilo la kupunguza muda wa Serikali kuwasilisha utetezi wake kutoka siku 14 zinazoelekezwa kisheria.
Awali Serikali kupitia kwa mwanasheria wa Serikali mkuu, Mark Mulwambo iliomba kuongezewa muda kutoka siku 14 za kisheria mpaka siku 21 kwa madai ya kufanya mashauriano baina ya Serikali na taasisi zake nyingine.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Sahel amesema mahakama haikushawishika na maombi ya Serikali ya kuongezewa muda kwa lengo la kushaurina.
“Kwa kuzingatia kwamba shauri hili limewasilishwa chini ya hati ya dharura na kwa kuwa lina maslahi kwa umma na kwa kuzingatia kwamba muswada huu umepangwa kusomwa bungeni kwa mara ya pili Januari 15, 2019 mahakama inatoa amri zifuatazo,” amesema.
“Mjibu maombi atawasilisha majibu yake akiambatanisha na hati ya kiapo ndani ya siku saba tangu siku ya kupewa nyaraka za shauri hili, yaani atawasilisha utetezi wake kabla au Januari 9, 2019. Usikilizwaji wa shauri hili utafanyika Januari 11 saa 3 asubuhi.”
Katika shauri hilo la Kikatiba namba 31 la mwaka 2018, waombaji wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachoeleza kuwa muswada wowote hauwezi kupingwa mahakamani.
Zitto na wenzake wanapinga muswada huo pamoja na mambo mengine wakidai kuwa unakiuka haki za kisiasa za binadamu kwa kuwa unaharamisha shughuli za kisiasa na kumpa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa, yakiwemo ya uongozi.