TUNDU LISSU KUANZA ZIARA BARANI ULAYA KUANZIA JUMATATU


Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili barani Ulaya kuanzia Jumatatu Januari 28, 2019.
****

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

ZIARA YA MWANASHERIA MKUU TUNDU LISSU (MB) ULAYA NA MAREKANI

Mwanasheria Mkuu wa Chama Mhe. Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili za Ulaya na Marekani kuanzia Jumatatu, Januari 28, mwaka huu, ambako mbali ya kufanya vikao kadhaa na viongozi wa kiserikali na jumuiya mbalimbali, pia atapata fursa ya kutoa mihadhara ya kitaaluma na kufanya mahojiano na vyombo vya habari.

Siku hiyo ya kwanza ya ziara yake, Mhe. Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, atakuwa nchini Ujerumani kwa siku mbili, ambako atakutana na baadhi ya maofisa wa Serikali pamoja na wabunge wa Bunge la Ujerumani.

Baadae Mhe. Lissu atazuru Makao Makuu ya Jumuiya ya Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji ambako atakutana na baadhi ya watendaji wa jumuiya hiyo, wabunge wa EU pamoja na wanadiplomasia wa mataifa mbalimbali wanaowakilisha nchi zao EU.

Baada ya Ubelgiji, Mhe. Lissu ataelekea Washington DC, Marekani kwa siku 10 ambapo mbali ya kukutana na Watanzania wanaoishi nchini humo, hususan katika maeneo ya Washington, Houston, Texas, Birmingham na Alabama, atakutana pia na Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pamoja na  Watendaji wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID). Halikadhalika atakutana na Kamati za mabunge yote mawili ya Marekani zinazohusika na Uhusiano wa Nje (Afrika).

Katika ziara hiyo, Mhe. Lissu atapata fursa ya kuwasilisha mada juu ya masuala mbalimbali katika taasisi kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na Center for Strategic and International Studies (CSIS) na The Atlantic Council and the World Resources Institute (WRI). Mhe. Lissu ana historia na taasisi ya WRI kwani aliwahi kuwa mmoja wa watafiti wake miaka ishirini iliyopita. 

Akiwa mjini Washington DC, Mhe. Lissu atakutana na kufanya mahojiano na baadhi ya vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa vilivyoko Mji Mkuu wa Marekani.

Mhe. Lissu atahitimisha ziara hiyo kwa kufanya mhadhara mkubwa wa umma katika Chuo Kikuu cha George Washington (GWU). Chuo hicho ni moja ya taasisi kongwe na kubwa za elimu ya juu nchini humo na duniani kwa ujumla.

Kutokana na umuhimu wa ziara hiyo kwa Chama, siasa za Tanzania na mapambano ya kutafuta mabadiliko ya kweli nchini kwa ujumla, siku ya Jumapili, Januari 27, mwaka huu, Mhe. Lissu atazungumzia baadhi ya masuala kuhusu ziara hiyo pamoja na maendeleo ya matibabu na hali ya afya yake.

Imetolewa leo Jumamosi, Januari 26, 2019 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527