HATMA YA UBUNGE WA TUNDU LISSU NDUGAI ATAKAPOVAA JOHO


Hatma ya ubunge wa Tundu Lissu itajulikana kuanzia Januari 29 wakati Job Ndugai atakapovaa “joho” la uspika kuongoza Mkutano wa 14 wa chombo hicho cha kutunga sheria.

Ndugai amemtaka Lissu arejee nyumbani kuendelea na majukumu yake ya kuwawakilisha wananchi wa Singida Mashariki, akisema hana kibali baada ya mbunge huyo kutoa tamko mwishoni mwa wiki akituhumu kuwepo na mpango wa kumvua ubunge.

Lissu yuko nchini Ubelgiji kumalizia matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma, ikiwa ni saa chache baada ya kuhudhuria kikao cha Bunge.

Baada ya shambulio hilo la Septemba 7, mwaka juzi alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa kwa ndege kwenda Nairobi, Kenya usiku wa siku hiyo.

Mkutano huo wa 14 wa Bunge la Kumi na Moja utaanza Januari 29, siku saba kuanzia leo, pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyehojiwa jana na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.

Majibizano kati ya Lissu na Spika Ndugai yamekuwa yakipamba moto siku hadi siku tangu alipotoa waraka alioupa jina la “Baada ya Risasi Kushindwa, Sasa Wanataka Kunivua Ubunge”. Katika waraka huo, Lissu anatuhumu uongozi wa Bunge na Serikali kuandaa mpango huo, jambo ambalo Ndugai amesema “ni uzushi”.

Jana, Mwananchi ilimuhoji tena Spika Ndugai kuhusu madai ya Lissu kuwa anafahamu taarifa za matatizo yake na kwamba alishiriki katika hatua za awali za kumuwezesha kupata matibabu, jambo ambalo alikubaliana nalo.

“Alipopata matatizo wote tulishuhudia na Bunge lilitimiza wajibu wake katika zile saa chache ambazo ni muhimu katika kuokoa maisha yake. Na hilo lilifanikiwa. Tunatambua kwamba mwenzetu aliumizwa na alikuwa hospitalini,” alisema Spika Ndugai.

“Ila sasa hivi tunavyoongea ametoka hospitali yuko huko aliko. Inaelekea ameruhusiwa. Amekuwa akitumia mwanya huo kuzunguka na kuchafua sifa ya nchi yetu. Kwani nani amempa ruhusa?

“Sasa nimwambie tu kwamba sisi tunamuhitaji maana mpaka sasa hajawahi kuniandikia chochote mimi kama kiongozi wake bungeni na wala daktari wake hajasema kitu. Kwa maana hiyo, mimi namuhesabu kama ni mtoro.”

Alipoulizwa sababu za muhimili huo kushindwa kumuhudumia Lissu licha ya familia yake kuandika barua mara nne, Ndugai alijibu kwa kifupi: “Hayo ya nyuma tuyaache. Atakapokuja mwenyewe tutayazungumza.”

‘Nilienda BBC nikitokea hospitali’

Na Tausi Mbowe, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527