VIGOGO TISA KUSHEREHEKEA KRISMASI GEREZANI

Huenda vigogo tisa wanaokabiliwa na kesi zilizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakasherehekea sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiwa rumande kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya upelelezi kutokamilika.

Lakini wengine kesi zao hazina dhamana na wengine wamefutiwa dhamana.

Miongoni mwa vigogo hao ni pamoja na Harry Kitilya na maofisa wa zamani wa benki ya Stanbic; Shose Sinare na Sioi Solomon wanaosota rumande kwa takribani miaka miwili na miezi minane kutokana na upelelezi wa shauri lao la utakatishaji fedha kutokamilika. Wote walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili Mosi, 2016.

Kitilya, ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), pia aliwahi kuwa kamishna mkuu wa TRA. Mbali ya Kitilya wamo pia mkurugenzi mkuu wa zamani wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Benhadard Tito; mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; wafanyabiashara Habinder Seth na James Rugemarila.

Wengine ni Yusuf Ali maarufu kama Shehe au Mpemba, Mohamed Mustafa Yusufali, Dk Ringo Tenga na mkurugenzi wa uthaminishaji almasi na vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo.

Na Hadija Jumanne, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527