BIASHARA YA UKAHABA TISHIO DODOMA...POLISI WATAHADHARISHA ONGEZEKO MAAMBUKIZI YA VVU


Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, limesema kasi ya biashara ya ukahaba inahatarisha usalama wa afya na kulifanya jiji hilo kuwa na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Ukimwi. 

Akizungumza jana na waandishi wa habari jiji Dododma kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa 64 kati yao wakiwamo 11 wa ukahaba, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilles Muroto, alisema kuwa jeshi hilo litaendelea kuwakamata watu hao kwa kuwa wanachafua taswira ya jiji hilo.

Kamata kamata ya watu wanaofanya biashara hiyo, ilianza Oktoba 9, mwaka huu na kukamata makahaba 22, wanaume watano waliokuwa wakiwanunua pamoja na wamiliki wanne wa maeneo yanayoruhusu biashara hizo.

Aidha, Oktoba 31, mwaka huu, jeshi hilo liliwakamata watu wengine 17 wanaotuhumiwa kufanya biashara hiyo.

"Watuhumiwa hawa wote watafikishwa mahakamani na jeshi letu litaendelea na msako wa kuwakamata makahaba wote jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa ndiye balozi wetu wa kupinga maambukizi mapya ya Ukimwi,hivyo hatuwezi kuendelea kuwavumilia hawa watu," alisema Muroto.

Alisema kumekuwa na ongezeko la biashara hiyo kwa kasi, hivyo ni vyema watu wakachukua tahadhari kujiepusha na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo.

Chanzo - Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527