MBIVU NA MBICHI LEO TUZO YA MCHEZAJI BORA WA DUNIA

Toleo hilo namba 63 la tuzo ya  Ballon d'Or linatarajiwa kufanyika Jijini Paris, Ufaransa leo Jumatatu Desemba 3 ambapo mshereheshaji atakuwa ni mchezaji wa zamani wa Ufaransa na klabu ya Tottenham Hortspurs, David Ginola.


Orodha ya wachezaji 30 ilishatangazwa na kuanza kupigiwa kura tangu miezi mitatu iliyopita, listi hiyo inaongozwa na Luca Modric ambaye ameonekana kufanya vizuri zaidi pengine kuliko wachezaji wengi waliotajwa katika listi hiyo, akishinda tuzo mbalimbali na klabu yake pamoja na zake binafsi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham Hortspurs, Modric amefurahia mwaka mzuri akiwa na klabu pamoja na nchi yake ambapo ameisaidia Real Madrid kushinda ubingwa wa Ulaya kwa mara ya nne katika miaka mitano na kisha kuiongoza timu ya taifa ya Croatia kucheza fainali ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

Croatia walipigwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mchezo wa fainali huko Moscow mapema katikati ya mwaka huu, lakini Modric aliimarisha sifa yake kama mchezaji bora zaidi duniani wakati wa mashindano hayo kwa kushinda kiatu cha dhahabu.

Modric pia alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa wanaume wa FIFA katika sherehe ya tuzo hizo Jijini London mnamo mwezi Septemba, akiwabwaga nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah wa Liverpool.

Pamoja na Ronaldo, Messi na Salah, mshindi wa Kombe la Dunia wa Ufaransa Kylian Mbappe, Antoine Griezmann na Raphael Varane pamoja na nyota wa Brazil, Neymar, ni miongoni mwa wachezaji walio katika orodha ya Ballon d'Or iliyotolewa  Oktoba mwaka huu.

Mchezaji Harry Kane na Gareth Bale wa Wales ndiyo wachezaji pekee wa Uingereza waliojumuishwa katika listi ya wanaowania tuzo hiyo.

Mbali na Ballon d'Or pia itatolewa tuzo ya kwanza kwa mchezaji bora chini ya miaka 21 ijulikanayo kama 'Kopa' ambapo wachezaji wanaopewa nafasi zaidi ni mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe na mlinzi wa Liverpool,  Trent Alexander-Arnold.

Ikumbukwe kuwa tuzo hii ya Ballon d'Or mchezaji wa zamani wa AC Milan na timu ya taifa ya Brazil, Kaka ndiye alikuwa mchezaji wa mwisho tofauti na Ronaldo na Messi kuwa mshindi wa Ballon d'Or, aliposhinda tuzo hiyo mwaka 2007, hivyo nyota hao wawili wanayo nafasi kubwa ya kuendeleza rekodi yao.
Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527