MHANDISI MATATANI KWA RUSHWA YA NGONO

Mhandisi wa Kampuni ya Mask and Sons ya jijini Dar es Salaam, Leonard Mkaka, amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za rushwa ya ngono.


Katika taarifa ya awali, iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Pilly Mwakasege, Mkaka alikamatwa juzi saa saba mchana katika nyumba ya wageni iliyopo Kibada, Kigamboni akiwa na mlalamikaji, tayari kwa kutekeleza azma yake.


Mwakasege alisema waliamua kumfuatilia mtuhumiwa huyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mlalamikaji ambaye alidai kuombwa rushwa ya ngono na mhandisi huyo ili amuwekee daraja (culvert) kwenye nyumba anayoishi.


“Mlalamikaji alikuwa ameomba awekewe culvert kufuatia miundombinu ya barabara kuelekea nyumbani kwake kuharibika kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea katika eneo hilo,” alisema.


Alisema ombi hilo lilifikishwa kwa mtuhumiwa ambaye ni mhandisi wa kampuni hiyo iliyopewa jukumu la kutengeneza miundombinu ya barabara na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, katika Kata ya Tuangoma Mtaa wa Masaki.


Alisema mtuhumiwa alianza kuomba rushwa ya ngono kwa mlalamikaji (jina limehifadhiwa) kuanzia Novemba 16 hadi Desemba 4 mwaka huu, alipokamatwa na maofisa wa Takukuru ambao walikuwa wakimfuatilia na kukusanya ushahidi katika kipindi hicho chote.


Mwakasege alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka chini ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007 mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post