Picha : BENKI YA NMB YATOA MSAADA WA STULI NA MEZA ZA MAABARA SHULE YA SEKONDARI MWANTINI SHINYANGA


Benki ya NMB imetoa msaada wa Stuli 32 na meza 8 za maabara zenye thamani ya Shilingi milioni tano ili kusaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi katika shule ya Sekondari Mwantini iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga. 



Msaada huo umekabidhiwa leo Alhamis Desemba 6,2018 na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko. 


Katamba alisema msaada huo wa stuli na meza ni sehemu ya ushiriki wa benki hiyo katika maendeleo ya jamii akibainisha kuwa ,changamoto za sekta ya elimu nchini kwa NMB ni jambo la kipaumbele kutokana na kwamba elimu ni uti wa mgongo wa taifa lolote duniani. 

“NMB tulipokea maombi kuwa mnahitaji stuli na meza za maabara,tulifarijika na kuamua kuja mara moja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto wetu katika shule hii”,alieleza. 

“Tunatambua kuwa kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka,kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni,tutaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wetu kuhakikisha changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi”,aliongeza Katamba. 

Hata hivyo alisema kwa mwaka 2018,NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu hivyo kuifanya benki ya NMB kuwa benki ya kwanza kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini. 

Kwa Upande wake,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko aliishukuru benki ya NMB kwa mchango huo mkubwa katika shule ya Mwantini hali ambayo itawafanya watoto wajifunze kwa vitendo masomo ya sayansi. 

“Tunawashukuru sana NMB kwa jitihada mnazofanya katika sekta ya elimu,serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto zote, ni lazima tushirikiane na wadau”,alisema Mboneko. 

“Wanafunzi someni kwa bidii ,epukeni vishawishi na kataeni kuolewa katika umri mdogo,someni masomo ya sayansi kwani Tanzania ya Viwanda itajengwa kama kutakuwa na wataalamu wa Sayansi”,aliongeza. 

Naye Diwani wa kata ya Mwantini,Majenga Samson aliitaka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kumalizia ujenzi wa jengo la maabara katika shule hiyo pamoja kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike. 

Hafla fupi ya makabidhiano hayo pia imehudhuriwa na Mwenyekiti wa ALAT taifa,mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje. 

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa kupokea msaada wa stuli na meza za maabara zenye thamani ya shilingi milioni 5 zilizotolewa na Benki ya NMB ili kusaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Mwantini - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko akiishukuru benki ya NMB kwa msaada wa stuli na meza za maabara katika shule ya sekondari Mwantini iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Wa pili kulia ni Diwani wa kata ya Mwantini Majenga Samson,akifuatiwa na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba na Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus.
 Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko akiwasisitiza wanafunzi kusoma masomo ya sayansi,kuepuka vishawishi na kukataa kuolewa katika umri mdogo.
Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba akizungumza wakati wa kukabidhi stuli 38 na meza 8 za maabara katika shule ya sekondari Mwantini.Alisema benki hiyo imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye elimu kwa kutoa madawati na viti na afya kutoa vitanda na magodoro pamoja na kusaidia pale majanga yanapotokea nchini.
Katamba akizungumza wakati wa kukabidhi stuli na meza za maabara.Alisema benki hiyo inayoongoza nchini kwa kuwa na matawi mengi ambayo ni 228,ATM zaidi ya 800 nchi nzima,NMB Wakala zaidi ya 6000 na wateja zaidi ya milioni 3 inaendelea kuboresha huduma za kibenki kwa njia ya mtandao ili kuwafikishia huduma za kibenki wananchi wengi zaidi.
Sehemu ya stuli na meza za maabara zilizotolewa na benki ya NMB kwa ajili ya wanafunzi katika shule ya sekondari Mwantini iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus akimkaribisha Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba ili akabidhi stuli 32 na meza 8 za maabara kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko kwa ajili ya shule ya sekondari Mwantini.
Kulia ni Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba akishikana mkono na  Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko wakati wa zoezi la kukabidhi stuli 32 na meza 8 za maabara kwa ajili ya shule ya sekondari Mwantini.Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa ALAT taifa,mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam ambaye pia ni Mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko akipokea stuli ya maabara kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje wakipokea moja kati ya stuli 32 kutoka benki ya NMB. Kulia ni Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko akisalimiana na wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini.
Picha ya pamoja wakati wa makabidhiano ya stuli na meza za maabara katika shule ya sekondari Mwantini.
Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus akimweleza jambo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko.
Meneja wa Benki ya NMB  Manonga,Baraka Ladislaus akitoa elimu kuhusu NMB Chipukizi Account kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini.
Awali Mkuu wa shule ya sekondari Mwantini,Rabanus Malele akitambulisha viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano ya stuli na meza zenye thamani ya shilingi milioni 5 zilizotolewa na benki ya NMB.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje akizungumza wakati makabidhiano ya stuli na meza za maabara.Aliomba serikali kumalizia ujenzi wa jengo la maabara katika shule ya sekondari Mwantini ambalo sasa halina milango wala madirisha.
Mwenyekiti wa ALAT taifa,mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam ambaye pia ni Mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga akizungumza wakati wa makabidhiano ya stuli na meza za maabara ambapo aliishukuru benki ya NMB kwa kutoa msaada huo kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini.
Diwani wa kata ya Mwantini Majenga Samson akiomba serikali kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini.
Maafisa wa benki ya NMB wakiwa katika chumba cha maabara katika shule ya sekondari Mwantini.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini wakiwa katika chumba cha maabara katika shule hiyo.
 Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko akitoa maagizo kwa viongozi baada ya kumalizika kwa zoezi la makabidhiano ya ya stuli na meza za maabara katika shule ya sekondari Mwantini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko akiwa katika picha ya pamoja na walimu,wanafunzi,viongozi wa benki ya NMB na viongozi mbalimbali.
Picha nyingine ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527