NISHATI JADIDIFU UKOMBOZI KWA UHIFADHI MAZINGIRA TANZANIA



Solar Panels during daytime: Photos by Mariana Proenca. 
Tanzania is set to develop Ngozi Geothermal Steam field.
Tree gray windmills: Photo by T. Chick McClure
Picha ya maandalizi ya umeme wa upepo Ikungi Singida.


Na Andrew Kuchonjoma - Songea 

Nishati Jadidifu ni neno ambalo halifahamiki na watu wengi hapa nchini jambo ambalo linakwamisha utekelezwaji wa dhima iliyopo katika neno hilo ambalo linashikilia uhai wa binadamu kwa kuwa linamaanisha uzalishaji wa nishati unaozingatia uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu. 

Neno Jadidifu ndilo linaonekena kuwa ngeni masikioni mwa Watanzania walio wengi kwani wengine wanauliza ndiyo kitu gani hicho? Wapo wanaosema ni kitu kinachojadilika na wapo wanaosema neno Jadidifu ni mbadala kwa maana inapotamkwa nishati jadidifu ni uzalishwaji wa umeme unaozingatia uhifadhi wa mazingira ambao unatokana na vyanzo ambavyo havina ukomo katika upatikanaji wake kama vile Jua, Maji, upepo, mvuke unaotoka ardhini (Geothermal) n.k lakini sio makaa ya mawe, mafuta (oil) na Gesi ambapo kitaalam wanaita Fossil Fuels. 

Kwa nini inaitwa Nishati mbadala ni kwa sababu nishati hiyo ndiyo inayoweza kutumika kwa lengo la kuhifadhi mazingira na hivyo kuondokana kabisa na uchafuzi wa mazingira kwenye adhi, maji, na anga ili kuepusha mabadiliko ya tabianchi kunakosababishwa na joto kali baada ya tabaka la anga lijulikanalo “ozone layer” kutobolewa kwa sababu ya ongezeko la Co2 inayozalishwa kutokana na shughuli za kibinadamu kama vile hewa inayozalishwa viwandani “indusrial Gases”. 

Kwa mantiki hiyo hata waandishi wa habari walio wengi hapa nchini Tanzania hawajui maana ya nishati jadidifu na ndiyo maana wanashindwa kuandika habari za nishati jadidifu (Renewable Energy ) na kama hao hawajui na ndiyo wanahusika moja kwa moja kuipasha habari jamii kwa maana ya kuelimisha je, wananchi wa kawaida watajua maana ya nishati jadidifu? 

Hivyo kama Wanazuoni hao walio wengi mikoani hawajui maana yake wananchi hawatajua kiundani mabadiliko ya tabianchi yanasababishwa na nini, kwa nini hali ya hewa inabadilika na hivyo ni vigumu kupata jamii inayobadilika kwa kuwa na mtizamo chanya kuhusu mazingira kwa maisha ya sasa na vizazi vijavyo. 

Nimeamua kutoa kidogo kati ya vingi nilivyojifunza kwenye mafunzo yaliyojulikana kama Renewable Energy Safari yaliyofanyika Arusha mwaka 2018 katika chuo cha MSTCDC cha ushirikiano wa Tanzania na Denmark kilichopo Usa River ambako waandishi 20 walioshinda fellowship ya Nishati Jadidifu inayoendeshwa na Nukta Africa kwa miezi sita itakayoisha mwakani 2019 mwezi mei walipatiwa mafunzo hayo. 

Prosper Magali mkurugenzi wa mradi na maendeleo ya biashara katika kampuni ya usambazaji umeme wa jua “Mini-Grid” ijulikanayo kwa jina la Ensol alieleza kwamba kuna umuhimu kwa waandishi wa habari kupata mafunzo ya uandishi wa habari za nishati jadidifu ili kumwezesha mwananchi wa kijijini ambako umeme haujafika kuona umuhimu wa nishati mbadala kama vile umeme jua kuwa unaweza kuwaongezea kipato. 

Akitolea mfano Magali alisema kwamba wao kama kampuni ya ukandarasi wa daraja la kwanza la umeme jua kupitia kampuni yao ya Ensol wametengeneza umemejua katika kijiji cha Mpale mkoani Tanga ambako wamewaunganisha watu 150 ingawa lengo lao ni kuwafikia watu 300. 

Alisema wakati wanaanza watu wa kijiji hicho walikuwa wanashangaa sana kwa kuwa wengine walikuwa hawajawahi kuuona umeme hivyo ilikuwa ni vigumu kuwapata hadi pale walipotoa elimu ya kutosha na sasa wanamuamko wa siku hadi siku kwani wameona manufaa yake ikiwa ni pamoja na watoto wao kupata muda wa kujisomea nyakati za usiku jambo ambalo awali halikuwepo. 

kwa kuanza matumizi hayo ya umeme wanakijiji hao wameacha kutumia kuni nyakati za usiku hivyo kwa hali ya kawaida hata ukataji miti kwaajili ya kuni umepungua. hivyo hapo sasa ndipo mwandishi wa habari anahitajika kujua ni kiasi gani cha nishati ya kuni kilikuwa kinatumika kwa siku na ni sawa na miti mingapi ilikuwa inakatwa kwa siku mara wiki, mwezi na mwaka mzima ili kujua ni hekari ngapi za miti zilikuwa zinateketea na hivyo kuchangia uharibifu wa mazingira. 

naye mwakilishi wa kampuni ya Mobisol iliyopo Arusha Sett Matemu wa idara ya masoko alisema Nishati Jadidifu haikwepeki kutokana na jinsi Dunia inavyokwenda hivyo cha msingi kwa wanahabari ni kujifunza na kupata data yaani takwimu ili kuweza kujua umeme jua umeweza kuwafikia wangapi wenye shida vijijini kama vile kwenye vituo vya afya, shule na umewezaje kukuza biashara kwa lengo la kumuondolea umasikini wa kipato mwananchi kule kijijini. 

kwa kutumia data alisema ndipo wananchi wataweza kujua ni hewa ya kaboni kiasi gani kimepungua ambayo ilikuwa inaharibu tabaka la anga “ozone layer” na ukataji miti umepungua kwa kiasi gani ikilenga kuhifadhi mazingira. 

kwa upande wake mwakilishi wa Hivors ambaye pia alikuwa mwezeshaji kwenye mafunzo hayo Maimuna Kabates raia wa Kenya alisema upo umuhimu sana wa waandishi kujengewa uwezo wa kuandika habari za nishati hususani nishati jadidifu kwa kuwa mahali penye umeme pana maendeleo na pasipokuwa na umeme hapana maenedeleo. 

Alisema endapo mwandishi wa habari atajengewa uwezo wa namna ya kuripoti habari za nishati jadidifu basi itakuwa ni ukombozi kwa wananchi kiuchumi, elimu, na mambo ya kidigitali kwani kuna maeneo wanahitaji kuangalia TV lakini wanashindwa kutokana na ukosefu wa umeme na hivyo wanashindwa kujua Duniani kinaendelea nini. 

hivyo alieleza mafunzo ya Energy Safari ni ufunguo wa kupata uelewa wa namna ya kuandika habari za nishati jadidifu kupitia fellowship inayoendeshwa na Nukta Afrika ambao watafundisha mambo ya data Journalism, digital journalism na mambo mengine muhimu ya uandishi wa habari wa sasa unaoendelea duniani. 

alieleza kwa kuwa hivi sasa kuna njia mpya inayotumika kupata wazo la habari za nishati jadidifu kama vile “PESTEL” P= Political, E=Economical, S= Social, T=Technological, E= Environmental na L= Legal ambapo mwandishi anapaswa kuandika habari zake za nishati jadidifu kwa kuangalia angle hizo. 

Kwa upande wake mkurugenzi wa Nukta Afrika Nuzulark Ndausen alisema waandishi wanapaswa kubadiliki kwani uandishi wa habari hivi sasa umebadilika kutoka kwenye maelelzo ya jumla na kwenda kwenye uandishi wa takwimu “Data Journalism” 

“Ili kuingia kwenye ulimwengu wa Data Journalism mwandishi anapaswa kupata mafunzo ya aina hiyo ili aweze kuendana na viwango vya kimataifa vinginevyo waandishi Tanzania tutabaki kamaq tulivyo kwa kuandika habari za alisema, alipongeza, akacheza ngoma na watu wakafurahi sana; so what?” alisema Ndausen.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527