MAPYA YAIBUKA MSOMI KUJIUA KWA KUJIRUSHA GHOROFANI...MSIBA PIA HAUJULIKANI ULIPO


Musa Ally (25), aliyejirusha juzi kutoka ghorofa ya tatu katika jengo la Rocky City Mall jijini Mwanza na kufa papo hapo si mkazi wa Kiloleni kama ilivyoelezwa awali.

Akizungumza na Mwananchi jana, Diwani wa Ibungilo, Yusuf Msoke alisema wananchi wa sehemu hiyo wanafahamika na iwapo kama kijana huyo angekuwa mkazi wa Kiloleni kama walivyoeleza polisi, wangekuwa wanamfahamu.

Juzi, Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Advera Bulimba alisema kijana huyo alionekana akiwa amelewa kupita kiasi na tangu Desemba 16 alikamatwa na kuwekwa Kituo cha Polisi Kirumba, lakini kilevi kilipopungua aliachiwa.

Bulimba alisema baada ya polisi kumwachia alikwenda kunywa tena pombe na baadaye kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya jengo hilo ambapo alikutwa na pombe kali na ugoro

Katika ufafanuzi wake, Msoke alisema ana shaka juu ya majina yaliyotumika kumtambulisha marehemu, akisema iweje msiba usijulikane hata ulipo.

“Huyu kwa kweli siyo wa hapa. Watu wangu wote wana utaratibu wa kutambuana katika daftari maalumu la wananzengo (wakazi). Kama ni wa hapa itafahamika tu hata kama siyo leo,” alisema Msoke.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiloleli ‘A’ inakodaiwa ndiko alikokuwa akiishi Musa, Edgeni Lutahiwa alisema hajawahi kusikia jina la marehemu. “Mimi niliona tu mitandaoni kuna mtu kajirusha kutoka ghorofani na baadaye ikaelezwa kuwa ni mkazi wa hapa, pengine ndugu zake wanaogopa kujitokeza,” alisema.

Justine Madereke, mkazi wa mtaa huo alisema hakumtambua marehemu.

Alisema, “Huwa (marehemu) anazunguka hapa sokoni muda wa mchana na anakuwa ni mlevi tu. Sasa kwa kuwa sisi hatumfahamu hatukuwa na nia wala haja ya kumdadisi.”

Katika maelezo yake, Bulimba alisema wakati polisi wakimhoji kabla ya kumwachia Musa alidai ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, na alilalamika kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kukosa kazi.

“Marehemu alidai kuwa ni msomi, hana kazi na pia ni yatima. Wakati Jeshi la Polisi wakichukua maiti hiyo ilikuwa na kijikaratasi kimeandikwa kwamba asilaumiwe mtu,” alisema Bulimba.

Na Jonathan Musa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527