RAISI MAGUFULI AFUNGUKA, KODI ZINAZOKUSANYWA NA TRA ZA KUUDHI,

Rais John Magufuli amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatakiwa kujitathmini kwanini watu wanakwepa kulipa kodi na kuamua kutumia wamachinga na wafanyabiashara wadogo kuwauzia bidhaa zao.

Ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 2, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa huduma za maji safi na maji taka katika kijiji cha Kimnyaki mkoani Arusha.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa na tabia ya kutumia wamachinga kuuza bidhaa zao ili wasilipe kodi.

"Mnaweka viwango vikubwa ambavyo havilipiki jambo ambalo linafanya wafanyabiashara kukwepa, hivyo ni bora kuweka viwango vidogo vinavyolipika na wengi kuliko kiwango kikubwa kinacholipwa na watu wachache," amesema.

Amesema baadhi ya kodi zinazokusanywa na TRA ni za kuudhi kwani licha ya kuwa aliwaagiza kukusanya kodi kila sehemu ila sio za dhulma.

Mbali na hilo aliwataka wamachinga kutumia vizuri fursa ya kufanya biashara kila sehemu waliyopewa ila sio katika kukwepa kodi.

"Serikali isiyokusanya mapato ni Serikali mfilisi, niwaombe sana wafichueni watu wenye tabia hiyo ili wasiwaharibie na muwe mnatoa elimu na sio kupeleka polisi kuwakamata wananchi wanaposhindwa kulipa kodi," amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527