CCM YAINGILIA KATI MALUMBANO YA BENARD MEMBE NA KATIBU MKUU WA CHAMA HICHO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kuhusu matokeo ya uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata 47 Tanzania Bara uliyofanyika tarehe 02 Desemba 2018 na kwamba CCM imepita bila kupingwa katika Kata 41 na katika Kata 6 ambako kumefanyika uchaguzi CCM imeshinda kwa kishindo.

Katika chaguzi hizi ambazo CCM imeendelea kuongoza inajivunia umakini mzuri wa kufuata Taratibu, Kanuni na Sheria za Nchi yetu, Sera nzuri, ahadi zinazotekeleka na siasa safi na uongozi bora.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuwashukuru watanzania na wanaCCM wote kwa kuendelea kukiamini na kukichagua na kwamba CCM itaendelea kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa haraka katika maeneo yao.

Aidha Chama kinapenda kuwafahamisha kuwa tarehe 17 hadi tarehe 18 Desemba 2018 Jijini Dar es salaam kutakuwa na vikao vya Chama vya kawaida vya Uongozi Taifa ambapo tarehe 17 Desemba 2018 kutakuwa na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na tarehe 18 Desemba 2018 Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitaketi. Hivyo taarifa hii inawajulisha wajumbe wote wa vikao husika kufika katika vikao hivyo.

CCM inapenda kuwafahamisha kuwa imefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wito alioutoa Ndg. Bashiru Ally Katibu Mkuu wa CCM kwa Ndg. Benard Membe ambaye ni Mwanachama wa CCM kama sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na Viongozi na Wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanaCCM. 

Tunapenda kutoa rai kwa watanzania kuwa wito wa Katibu Mkuu ulikuwa ni wito wa kawaida wa Kiongozi wa CCM kwa mwanachama wa CCM, hivyo uzushi, uchonganishi, fitina na uvumi mwingine wowote unaoendelea hasa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya Magazeti yenye hila mbaya, wana CCM na Umma wa watanzania wanaombwa waupuuze.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawataka wana CCM na watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa na umoja, mshikamano na upendo zaidi katika kipindi hiki ambacho Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anandelea kutuongoza katika Mageuzi makubwa ya kiuchumi na ya kimaendeleo kwa watanzania wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527