KAMANDA WA POLISI APEWA VITISHO NA WASIOJULIKANA...WADAI WATAMHAMISHA MKOA

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Pwani (ACP) Wankyo Nyigesa anadaiwa kutishiwa na watu wasiofahamika kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) kuwa watamhamisha kwenye mkoa huo kutokana na kuzuia kuingiza bidhaa za magendo kwenye bandari bubu.

Licha ya kitisho hicho amesema,hawezi kulegeza uzi kwani shughuli hizo zinasababisha nchi kukosa mapato kwa kukwepa ushuru.

Akizungumza kwenye kituo cha polisi wilaya ya Bagamoyo mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo baada ya kufanikiwa kukamata bidhaa mbalimbali ikiwemo madumu ya mafuta ya kula 4,311 ya lita 20 kila moja na mafuta ya dizeli madumu 52 kwenye oparesheni zinazoendelea mkoani humo.


“Kwa siku za hivi karibuni mimi pamoja na watendaji wenzangu akiwemo ofisa upelelezi wa mkoa tumekuwa tukitumiwa jumbe za vitisho kupitia simu”


“Nitafanya kazi kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa, IGP na Rais hivyo siko tayari kufanya kazi kwa maelekezo ya watu wengine ambayo ni kwa maslahi ya mtu binafsi bali kwa maslahi ya nchi”


“Sitishwi na mtu wala sms eti watatuhamisha ama watatupeleka Mlingotini waambieni meseji zao tunazo ,tunazifanyia kazi na tumechukua namba za hawa tuliowakamata kutokana na operesheni hizi kama ni miongoni mwao tutawachukulia hatua kali “alieleza Nyigesa.


Nae mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema lazima vyombo vinavyohusika vifuatilie jambo hili ikiwa ni pamoja na mamlaka ya chakula na dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA).


”Kila mamlaka hapo inapaswa kuhakiki bidhaa hizo ili kujiridhisha kuwa bidhaa hizi zimeingizwa nchini kwa kufuata taratibu ??na ile ya chakula na dawa kuangalia kama mafuta hayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu”alisema Ndikilo.


Katika msako huo pia vifaa vya ujenzi marumaru katoni 200, friji 16, pikipiki moja isiyokuwa na namba bangi kete 512 na pombe ya moshi lita 16 vilikamatwa na watuhumiwa 17 wanaotuhumiwa kuhusika na matukio hayo wanashikiliwa.
Na Mwamvua Mwinyi,pwani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527