HOTUBA YA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2019/20


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/2020.
 *****

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO
YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
NA MWONGOZO WA MAANDALIZI
YA MPANGO NA BAJETI
YA MWAKA 2019/20


UTANGULIZI

1.                  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kutoa maoni na ushauri kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kuboresha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/20.

2.                  Mheshimiwa Spika, kinachowasilishwa sasa mbele ya Bunge lako Tukufu ni kwa mujibu wa Kifungu cha 94  cha Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2016 kinachoelekeza Serikali kuwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata.

3.                  Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kinajumuisha mapitio ya hali ya uchumi; utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/18 na robo ya kwanza ya mwaka 2018/19; maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2019/20; ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20; mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa; na vihatarishi vya utekelezaji wa Mpango. Aidha tumeambatanisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano 2016/17 - 2018/19.

4.                  Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali 2019/20 - 2021/22 kimeainisha masuala muhimu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi na Mashirika ya Umma wakati wa kuandaa bajeti zao za mwaka 2019/20.

5.                  Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya ninayowasilisha yamezingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 - 2020/21; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Vilevile, maandalizi ya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo yamezingatia sera, mikakati na progamu mbalimbali za maendeleo ya kisekta zikiwemo: Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili; Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji; Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Afya; Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta Ndogo ya Umeme wa Mwaka 2016; Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu 2016/17 – 2020/21; Mkakati Jumuishi wa Kuendeleza Viwanda 2025; na Mpango Kabambe wa Sekta ya Utalii wa Mwaka 2006. Hivyo, ni vema Waheshimiwa Wabunge watakaposoma vitabu vya Mwongozo na Mapendekezo ya Mpango warejee pia mikakati na programu za kisekta.

6.                  Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ushauri na maoni yatakayotolewa katika kikao hiki cha Bunge yatazingatiwa kikamilifu katika kuandaa rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 utakaowasilishwa Bungeni tarehe 11 Machi 2019 kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge. Aidha, ushauri wa Waheshimiwa wabunge utatumika kuboresha Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/20. Hivyo, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge katika nafasi yenu ya uwakilishi wa wananchi, mtumie weledi na uzoefu wenu katika kutoa maoni, ushauri kuhusu maeneo muhimu na miradi inayopaswa kuzingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20.

MWENENDO WA VIASHIRIA VYA UCHUMI

7.                  Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa  Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.9 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 3.7 mwaka 2017. Hata hivyo, ukuaji huu unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mikopo na gharama zake na mabadiliko ya bei za bidhaa katika soko la dunia. Aidha, kati ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania na Rwanda zinatarajiwa kuwa na viwango vya juu vya ukuaji wa asilimia 7.2 mwaka 2018, zikifuatiwa na Kenya (asilimia 5.5); Uganda (asilimia 5.2); na Burundi (asilimia 0.1).

8.                  Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilifanya zoezi la mapitio ya kubadilisha mwaka wa kizio (base year) kwa Pato Ghafi la Taifa kutoka mwaka 2007 na kuwa mwaka 2015. Zoezi hili ni utekelezaji wa mapendekezo ya Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa ambayo inashauri Nchi Wanachama kufanya zoezi hili kila baada ya miaka mitano. Hivyo, takwimu zilizotumika katika kitabu cha Mpango, Mwongozo na taarifa hii zimezingatia mwaka wa kizio wa 2015.

9.                  Mheshimiwa Spika, kutokana na zoezi hilo, mabadiliko yaliyojitokeza ni pamoja na: kuongezeka kwa Pato Ghafi la Taifa kwa asilimia 6.3; kubadilika kwa uwiano wa viashiria vinavyopimwa kwa Pato Ghafi la Taifa ikijumuisha Mapato ya kodi, Nakisi ya bajeti na Deni la Serikali; viwango vya ukuaji; na mchango wa sekta katika Pato Ghafi  la Taifa. Kwa takwimu hizo za mwaka wa kizio wa 2015, Pato Halisi la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2013 - 2017). Kwa mwaka 2017, Pato la Taifa limeendelea kukua kwa kiwango kikubwa cha asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 7.0 kwa mwaka 2016. Kwa ukuaji huo Tanzania imeendelea kuongoza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikifuatiwa na nchi za Rwanda (asilimia 6.1); Kenya (asilimia 4.8); Uganda (asilimia 4.5); na Burundi (asilimia 0.0).

10.             Mheshimiwa Spika, katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na asilimia 5.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2017. Shughuli za kiuchumi ambazo zilikua kwa kiwango kikubwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 ni pamoja na: ujenzi (asilimia 20); habari na mawasiliano (asilimia 18.3); usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (asilimia 9.2); na kilimo (asilimia 7.1).

11.             Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa umechangia kupungua kwa umaskini. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wa mwaka 2015/16 ulionesha kuwa idadi ya watanzania wanaoishi chini ya mstari wa umaskini ilipungua kufikia asilimia 26.3 ikilinganishwa na asilimia 28.2 mwaka 2012. Utafiti mpya wa Matumizi ya Kaya Binafsi unaendelea hivi sasa na utafiti huo unatarajiwa kukamilika Machi 2019 na kutupatia hali halisi ya viwango vya umaskini. Aidha, wastani wa umri wa kuishi kwa Tanzania Bara umeongekeza kutoka wastani wa miaka 64.3 mwaka 2017 na unatarajiwa kuongezeka hadi wastani wa miaka 64.9 mwaka 2018.

12.             Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kuwa chini ya asilimia 5 kwa takribani kipindi chote cha mwaka 2017/18. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,483.9 mwishoni mwa mwezi Juni 2018, iliyokuwa na uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 5.6. Katika kipindi hicho, thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani iliendelea kuwa tulivu. Wastani wa mwenendo wa ubadilishaji Shilingi dhidi ya dola ya Marekani ulikuwa kati ya Shilingi 2,231.17 na Shilingi 2,264.97 kwa dola moja ya Marekani, ikilinganishwa na kati ya Shilingi 2,171.0 na Shilingi 2,230.1 kwa dola moja ya Marekani katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/17.

13.             Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni 2018 Deni la Taifa lilifikia dola za Marekani milioni 27,774.86 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 25,350.76 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.6.  Matokeo ya hivi karibuni ya uchambuzi wa Deni la Taifa, yameonesha kuwa deni la Taifa lipo chini ya ukomo wa hatari na ni himilivu. Viashiria vyote vya athari za madeni vimeendelea kuwa katika wigo unaokubalika kimataifa. Katika kipindi cha mwaka 2017/18, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yalikuwa dola za Marekani milioni 8,949.40 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,701.7 mwaka 2016/17, sawa na ongezeko la asilimia 2.8. Hii ilitokana na ongezeko la thamani ya mauzo ya mazao ya korosho, karafuu, tumbaku, chai na mkonge; pamoja na kuimarika kwa bei za dhahabu katika soko la Dunia.

14.             Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini umeendelea kuimarika. Katika msimu wa 2017/18, uzalishaji ulifikia tani milioni 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.3 ya chakula kwa kipindi hicho. Kutokana na uzalishaji huo, nchi ilikuwa na ziada ya tani milioni 2.6 za mazao yote ya chakula na hivyo, kujitosheleza kwa asilimia 120.

15.             Mheshimiwa Spika, baadhi ya viashiria vya sekta ya kibenki vilivyokuwa vimetetereka mwaka 2017 kwa sababu mbalimbali vimeanza kuimarika baada ya Serikali kuchukua hatua za kuongeza ukwasi ikiwa ni pamoja na Benki Kuu kushusha riba yake (discount rate). Kufuatia hatua hizo, mikopo kwa Sekta Binafsi imeanza kuonesha mwenendo unaoridhisha ambapo hadi kufikia Juni 2018 ilikua kwa asilimia 4.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.3 Juni 2017. Riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja zilipungua hadi wastani wa asilimia 10.52 ikilinganishwa na asilimia 11.66 mwaka 2016/17.  Hata hivyo, viwango vya riba ya mikopo ya mwaka mmoja ilifikia asilimia 18.48, ikilinganishwa na asilimia 15.49 mwaka 2016/17, hivyo kusababisha tofauti kati ya riba ya amana na mikopo ya mwaka mmoja kuongezeka hadi asilimia 7.98 mwaka 2017/18 kutoka asilimia 3.83 mwaka 2016/17.  Kuongezeka kwa riba ya mikopo kulitokana na tahadhari zilizochukuliwa na benki za biashara ili kudhibiti mikopo chechefu na hivyo kuongeza gharama kwa wakopaji, hali ambayo inaweza kuathiri uwekezaji katika shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi. Maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi yanapatikana katika Sura ya Pili, Sehemu ya Kwanza ya kitabu cha Mwongozo na Sura ya Pili ya kitabu cha Mapendekezo ya Mpango.

Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2017/18

16.             Mheshimiwa Spika, Mapato ya ndani katika mwaka 2017/18 yalifikia Shilingi bilioni  17,944.9 sawa na asilimia 90 ya lengo la Shilingi bilioni 19,977.0. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 15,191.0 zilitokana na Mapato ya Kodi, sawa na asilimia 89 ya lengo; Shilingi bilioni 2,212.4 zilitokana na Mapato yasiyo ya Kodi, sawa na asilimia 101 ya lengo; na Shilingi bilioni 541.5 zilitokana na mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, sawa na asilimia 79 ya lengo.

17.             Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu iliyotolewa ilikuwa Shilingi bilioni 2,466.0 sawa na asilimia 62 ya makadirio ya Shilingi bilioni 3,971.1. Mikopo iliyopatikana kutoka ndani na nje ni Shilingi bilioni 7,055.8, sawa na asilimia 90.9 ya lengo la Shilingi bilioni 7,763.9. Kati ya mikopo hiyo, Shilingi bilioni 1,351.5 ni kutoka vyanzo vya nje na Shilingi bilioni 5,704.4 ni kutoka vyanzo vya masoko ya ndani. Kati ya mikopo ya ndani, Shilingi bilioni 4,835.2 zilitumika kulipia Mtaji wa Deni la Ndani (Rollover) na Shilingi bilioni 869.2 ni Mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia bajeti ya Maendeleo.

18.             Mheshimiwa Spika, matumizi halisi ya Serikali yalifikia Shilingi bilioni 25,321.7 sawa na asilimia 80 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi bilioni 31,711.9. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 18,778.5 zilikuwa ni matumizi ya kawaida sawa na asilimia 93 ya lengo la Shilingi bilioni 20,279.3 na Shilingi bilioni 6,543.2 zilikuwa ni matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 57 ya  bajeti ya Shilingi bilioni 11,432.7. Matumizi ya fedha za maendeleo hayajumuishi baadhi ya fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja (D-funds) kwenye utekelezaji wa miradi ambazo hazikupita kwenye Mfumo wa Malipo wa Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu za kiuhasibu zitakapokamilika.

Utekelezaji wa Baadhi ya Miradi ya Maendeleo Mwaka 2017/18 na Robo ya Kwanza ya Mwaka 2018/19

19.             Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2017/18 na robo ya kwanza ya mwaka 2018/19 ni pamoja na:
(i)                Mradi wa kufua Umeme Unaotokana na Nguvu ya Maji katika Mto Rufiji MW 2,100: kuendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kuwezesha Mkandarasi kuanza kazi kwa wakati. Kazi zilizotekelezwa ni: ujenzi wa Njia ya Umeme wa Msongo wa kV 33 kutoka Msamvu  hadi eneo la mradi ambapo sehemu za Msamvu – Pangawe (km 14) na Dakawa – Mpakani mwa Pori la Akiba Selous (km 8.5) zimekamilika kwa asimilia 100 na kukamilika kwa asimilia 100 ya ujenzi wa Kituo cha Kupozea Umeme Pangawe; kukamilika kwa asilimia 100 kwa kazi ya kufikisha maji kwenye kambi za ujenzi, na kuendelea na kazi ya kufikisha maji Stesheni ya Reli ya TAZARA ya Fuga; kukamilika kwa asilimia 55 kwa kazi ya ukarabati na ujenzi wa nyumba zilizokuwa kambi ya RUBADA na kuendelea na uthamini wa mali zisizohamishika; kukamilika kwa asilimia 60 ya ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi – Mvuha – Kisaki – Mtemere Junction (km 178.39) na kukamilika kwa asilimia 60 ya ujenzi wa barabara ya Kibiti - Mloka – Mtemere – Matambwe Junction – Mto Rufiji (km 210); na kukamilika kwa mifumo ya mawasiliano mbadala kwenye eneo la mradi. Aidha, upembuzi yakinifu wa awali wa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme (Rufiji hadi Chalinze) umekamilika.

(ii)             Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Standard Gauge: kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) ujenzi wa reli umeanza na umefikia asilimia 24. Kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa njia, madaraja, utengenezaji wa mataruma na ujenzi wa miundombinu ya umeme. Aidha, kazi ya kutandika kilometa 60 za reli imeanza.

Kuhusu kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa kazi ya kutafuta mwelekeo wa njia; na kuendelea kufanya uthamini wa ardhi pamoja na mali. Aidha, Serikali inaendelea na taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu zilizosalia za Makutupora – Tabora (km 295), Tabora – Isaka (km 133), Isaka – Mwanza (km 250), Tabora – Uvinza – Kigoma, na Kaliua – Mpanda – Karema na Isaka – Rusumo (km 371). 
(iii)           Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: kununuliwa kwa ndege moja aina ya Bombadier Q 400 na moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner; kukamilika kwa sehemu ya malipo ya ununuzi wa ndege 2 aina ya A220-300 ambazo zinatarajiwa kuwasili Novemba, 2018 na Boeing 787-8 Dreamliner moja inayotarajiwa kuwasili mwaka 2020. Aidha, shughuli zinazoendelea ni pamoja na: ukarabati wa jengo la ofisi za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); utafutaji wa masoko ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa ofisi katika maeneo ya kimataifa ikujumuisha Bombay, Bujumbura, Guangzhou na Entebbe; na kuboresha miundombinu ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na mtandao wa mawasiliano ya simu. Aidha, ATCL imeanza kutoa huduma za usafiri kwa miji ya Bujumbura - Burundi na Entebbe – Uganda kuanzia Agosti 2018.

(iv)           Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga: kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi; kukamilika kwa tathmini za kijiolojia katika eneo la Chongoleani yatakapojengwa matenki na gati la kupakia mafuta; kuridhiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda; na kuendelea na majadiliano ya mkataba wa ubia.

(v)             Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: kuendelea na majadiliano ya mikataba kati ya Serikali na Wawekezaji wa Mradi wakiongozwa na Kampuni ya Shell - Tanzania na Statoil; kuendelea kuandaa mpango wa kuendeleza vitalu vya baharini; kuandaa mpango wa kushirikiana na wadau (stakeholders engagement plan) wa eneo la mradi; na kuendelea na mchakato wa kumpata Mshauri Mwelekezi (Transaction Advisor).

(vi)           Makaa ya Mawe (Mchuchuma) na Chuma (Liganga): kukamilika kwa taarifa ya awali ya Timu ya Majadiliano iliyopewa jukumu la kuchambua vivutio vilivyoombwa na Mwekezaji pamoja na kuainisha maeneo ya mikataba ya mradi yanayokinzana na sheria na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Serikali. Aidha, Timu ya Majadiliano ya Serikali inaendelea kufanya uchambuzi wa kina kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unakuwa na maslahi kwa Taifa.

(vii)        Uendelezaji wa Kanda Maalum ya Uwekezaji Bagamoyo: kufuatia kukamilika kwa  makubaliano ya awali ya utekelezaji wa mradi, Timu ya Serikali ya Majadiliano inaendelea na  majadiliano ya kina ya mikataba kuhusu uendelezaji wa eneo hilo na wawekezaji. Aidha,  majadiliano hayo yamechukua muda mrefu kutokana na kuwepo kwa vipengele vyenye masharti magumu yasiyo na maslahi kwa Taifa.

(viii)      Miradi ya Umeme: utekelezaji wa miradi ya kufua umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati vikiwemo maji na gesi unaendelea. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kufua umeme unaotokana na nguvu ya maji Ruhudji MW 358 (Serikali inaendelea na majadiliano na wafadhili ili kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza Mradi), Mradi wa kufua Umeme unaotokana na nguvu ya maji Malagarasi MW 45 (kuendelea na kudurusu upembuzi yakinifu wa mradi) na Mradi wa kufua Umeme unaotokana na nguvu ya maji Rusumo MW 80 (ujenzi umeanza);  miradi ya kufua umeme wa gesi Mtwara MW 300 (upembuzi yakinifu unaendelea) na mradi wa Somanga Fungu MW 330 (upo hatua ya ukamilishaji wa upembuzi yakinifu). Aidha, kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, vijiji 557 vimeunganishiwa umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA Phase III). Vile vile, mradi umewezesha taasisi 903, shule 1,983 maeneo ya biashara 1,743 na maabara za tiba 19 kuunganishwa umeme.

(ix)           Miradi ya Viwanda: (a) kuimarisha Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kwa kutengeneza mashine 64 zikiwemo za kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha mbogamboga na kukata majani; ujenzi wa mitambo 55 ya biogas; kubuni teknolojia mpya kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa na kukamilika kwa tafiti tatu zinazohusiana na matumizi ya nishati mbadala ya biogas(b) kuendeleza mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka - Arusha kwa kukamilisha upimaji wa ardhi  na uthamini wa mali za wananchi  ili kujua kiasi cha fidia kitakachohitajika; (c) kuimarisha mradi wa Kuunganisha Matrekta TAMCO - Kibaha ikijumuisha kuagizwa kwa vipande (Semi Knocked Down - SKD) kwa ajili ya kuunganishwa ili kupata matrekta 727; na kuunganisha matreka 420, majembe 95 na haro (harrow) 195; na (d) kuimarisha Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO) kwa kubuni mashine ya kutengeneza tofali zinazozuia upotevu wa joto, mtambo wa kusindika na kusafisha mafuta ya kula, mtambo wa kuzalisha umeme kutokana na nguvu ya maji na usimikaji wa mitambo wa kuzalisha umeme (kW 20) kutokana na nguvu za upepo na jua katika Kituo cha Olduvai Gorge – Ngorongoro.

(x)              Ujenzi wa Barabara za Juu (Flyovers) jijini Dar es Salaam: ujenzi wa Mfugale Flyover (TAZARA) umekamilika na kuanza kutumika. Vile vile, ujenzi wa Interchange ya Ubungo unaendelea.

(xi)           Ujenzi wa Meli katika Maziwa Makuu: (a) kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili; na kufikia hatua za mwisho za ujenzi wa meli moja yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika ziwa Nyasa unaotarajiwa kukamilika Desemba 2018 (b) kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa meli mpya katika ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambapo mkandarasi yupo katika hatua za awali za kuanza ujenzi; na mkataba wa ujenzi wa chelezo kwa ajili ya kujengea meli umesainiwa; na (c) kufikia hatua za mwisho za kusaini mkataba wa ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika ziwa Tanganyika.

(xii)         Viwanja vya Ndege: ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) la Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (Dar es Salaam) umefikia asilimia 78. Aidha, ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Kilimanjaro umekamilika na Kiwanja cha Mwanza umefikia asilimia 70.

(xiii)      Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Hadi Juni 2018, mtandao wa barabara za lami nchini ulifikia kilomita 8,298.12 kwa barabara kuu na kilomita 1,687 kwa barabara za mikoa. Aidha, madaraja makubwa yanayoendelea kujengwa ni pamoja na daraja la Mara (Mara) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 81.3, Sibiti (Singida) asilimia 79.8, Lukuledi (Lindi) asilimia 70, Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 65, Mlalakuwa (Dar es Salaam) asilimia 64, Magara (Manyara) asilimia 9 na Momba (Songwe) asilimia 7.5. Aidha, kwa daraja la Selander (Dar es Salaam)  na Wami (Pwani), mikataba ya ujenzi imesainiwa.

(xiv)      Uendelezaji wa Bandari: katika bandari ya Dar es Salaam utekelezaji umefikia asilimia 35 ambapo, uwekaji nguzo za msingi katika gati Na. 1 umekamilika; na ujenzi wa sakafu ngumu chini ya maji katika gati la kupakua na kupakia magari (Roll on Roll off  - Ro-Ro) unaendelea. Aidha, katika bandari ya Tanga, ukarabati wa maegesho, sehemu ya kupakulia shehena na barabara kuelekea lango Na. 2 umefikia asilimia 76 na ujenzi wa gati la mita 300 katika bandari ya Mtwara umefikia asilimia 30.


20.             Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2017/18 na robo ya kwanza ya mwaka 2018/19 yameainishwa katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Tatu).

MAFANIKIO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2018/19

21.             Mheshimiwa Spika, yapo mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano (2016/17 – 2018/19). Mafanikio hayo yanajumuisha yafuatayo:
    (i)            Ukuaji wa Uchumi: kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Taifa, ambapo uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 mwaka 2017 kutoka ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2016 na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kuwa katika wastani wa kiwango cha tarakimu moja, chini ya asilimia 5.0.


 (ii)            Mapato ya Kodi na Yasiyo ya Kodi: mapato ya kodi yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 12,434 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 15,191 mwaka 2017/18 na mapato yasiyo ya kodi yaliongezeka pia kutoka Shilingi bilioni 1,188 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 2,212.4 mwaka 2017/18. Aidha, ongezeko la mapato yasiyo ya kodi lilitokana na kuimarika kwa ufuatiliaji na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato hususan Wizara ya Madini (kutoka Shilingi bilioni 207.9 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 301.2 mwaka 2017/18), Ofisi ya Msajili wa Hazina (kutoka Shilingi bilioni 243.4 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 803.5 mwaka 2017/18), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (kutoka Shilingi bilioni 73.3 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 92.2 mwaka 2017/18) na Idara ya Uhamiaji (kutoka Shilingi bilioni 115.3 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 159.3 mwaka 2017/18).

(iii)            Ulipaji wa Madai: Serikali ililipa jumla ya Shilingi bilioni 2,288.9 za madai yaliyohakikiwa ya wakandarasi, watoa huduma, wazabuni, watumishi wa umma na madai mengineyo. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 1,611.0 zililipwa kwa wakandarasi, shilingi bilioni 144.6 kwa watoa huduma, shilingi bilioni 218.3 kwa wazabuni, Shilingi bilioni 285.9 kwa watumishi wa umma na Shilingi bilioni 29.1 kwa madai mengineyo.

(iv)            Barabara: mtandao wa barabara kuu za lami uliongezeka kutoka kilomita 7,646 Juni 2016 hadi kilomita 8,298.12 Juni 2018 na mtandao wa barabara za mikoa nao uliongezeka kutoka kilomita 1,398 hadi kilomita 1,687 kwa kipindi hicho. Aidha, ujenzi wa Barabara ya juu ya Mfugale Flyover (TAZARA) ulikamilika na kuanza kutumika na ujenzi wa Interchange ya Ubungo unaendelea.


 (v)            Reli: ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge umeanza, ambapo kwa awamu ya kwanza ya Dar es Salaam – Morogoro (km 300) ujenzi umefikia asilimia 24. Maandalizi ya ujenzi kwa sehemu ya Morogoro – Makutupora (km 422) nayo yameanza. Faida zitakazotokana na kukamilika kwa reli hii ni pamoja na: kupungua kwa muda wa kusafirisha abiria na mizigo; kuongezeka kwa kiwango cha usafirishaji wa abiria na mizigo; kuongezeka kwa mapato ya Serikali; kuongezeka kwa fursa za ajira; na kupanuka kwa biashara katika vijiji na miji inayopitiwa na reli hiyo.  Vile vile, Serikali imeendelea kuboresha reli ya kati inayotumika sasa ambapo mafanikio yaliyopatikana  ni pamoja na kuwezesha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mwanza (Mwanza South Port) kwenda Bandari ya Port Bell – Uganda ambapo katika mwaka 2017/18 wastani wa shehena ya mizigo ya tani 200,000 ilisafirishwa.

(vi)            Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: ndege mpya tatu (3) aina ya Bombadier Q 400 na moja (1) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner zilinunuliwa na kuanza kufanya kazi. Vile vile, sehemu ya malipo ya ndege mbili (2) aina ya A220 – 300 zinazotarajiwa kuwasili Novemba 2018 na moja (1) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner inayotarajiwa kuwasili mwaka 2020 yamefanyika. Kutokana na kuboreshwa kwa ATCL, idadi ya mikoa inayohudumiwa na ndege za ATCL imeongezeka na kufikia 10. Mikoa hiyo ni: Dar es Salaam, Kagera, Mbeya, Kigoma, Ruvuma, Mtwara, Dodoma, Tabora, Kilimanjaro na Mwanza. Aidha, Shirika pia linatoa huduma Zanzibar. Vile vile, Shirika limeanzisha ofisi katika miji ya Mumbai, Bujumbura, Guangzhou na Entebbe.

(vii)            Viwanja vya Ndege: ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria na miundombinu yake katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umefikia asilimia 78. Aidha, upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umefikia asilimia 70 na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro umekamilika. Upanuzi huu umewezesha kuongezeka kwa: abiria na mizigo; mapato ya Serikali; ajira; biashara za hoteli na maduka; na idadi ya watalii.

(viii)            Bandari: ujenzi wa gati la kupakua na kupakia magari (Roll on Roll off  - Ro-Ro) na upanuzi wa gati Na. 1 katika bandari ya Dar es Salaam umefikia asilimia 35, na upanuzi wa bandari za Tanga na Mtwara umefikia asilimia 76 na 30 kwa mtiririko huo. Kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha kuongezeka kwa uwezo wa bandari kuhudumia magari kati ya 300,000 hadi 500,000 kwa mwaka; kupungua kwa muda wa kupakua magari na hivyo kuongeza ufanisi wa bandari; kuongezeka kwa mapato ya Serikali; na kuhimili ushindani kutoka bandari za nchi jirani.


(ix)            Kilimo: kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo kiliongezeka kufikia asilimia 7.1 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2016. Ukuaji huu umewezesha kuongezeka kwa usalama wa chakula, kupungua kwa mfumuko wa bei ya chakula kufikia asilimia 3.8 Juni 2018 ikilinganishwa na asilimia 9.8 Juni 2017 na kuongezeka kwa mapato ya mauzo ya bidhaa asilia nje ya nchi kutoka dola za Marekani milioni 866.4 mwaka 2016/17 kufikia  dola milioni 1,152.4 mwaka 2017/18, sawa na ongezeko la asilimia 33. Vile vile, upatikanaji wa mbegu bora uliongezeka na kufikia tani 51,700.5 mwaka 2017/18 kutoka tani 36,482 mwaka 2015/16, na tani 435,178 za mbolea zilinunuliwa na kusambazwa katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na tani 302,450 zilizonunuliwa katika mwaka 2015/16. Aidha, katika kuimarisha Ushirika na Masoko ya Mazao, Vyama vya Ushirika viliongezeka kutoka 7,888 mwaka 2015 hadi 10,990 mwaka 2017.
  (x)            Huduma za Afya: kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa Hospitali 10 za Wilaya, Vituo vya Afya 295 na nyumba za watumishi wa afya 306. Aidha, bajeti ya ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/18. Kuanza kutoa huduma ya kupandikiza figo kwa wagonjwa 28 na hivyo kupunguza gharama kwa wastani kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 20 kwa mgonjwa mmoja endapo angepelekwa nje ya nchi. Vile vile, Serikali imeanzisha huduma ya kupandikiza vifaa vya kusikia (Cochlear Implant) kwa watoto ambapo jumla ya watoto 11 wamepatiwa huduma hiyo na hivyo kuokoa shilingi milioni 64 kwa mtoto mmoja endapo angepata huduma hii nje ya nchi.

(xi)            Nishati: uzalishaji wa umeme umeongezeka kutoka MWh 6,950,280 mwaka 2016/17 hadi MWh 7,010,590 mwaka 2017/18 ambao umewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongezeka kwa idadi ya wananchi waliounganishiwa umeme ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2018 jumla ya vijiji 5,181 tayari vimeunganishiwa umeme. Aidha, shughuli za kiuchumi pia zimeongezeka; vilevile, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji mto Rufiji - MW 2,100 umeanza; Pia, maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Kusafirishia Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga yamekamilika.

(xii)            Huduma za Maji: miradi 1,595 ya maji vijijini imekamilika, ikiwa na jumla ya vituo vya kuchotea maji 126,610 na uwezo wa kuhudumia wananchi 31,652,500.

(xiii)            Viwanda: Serikali iliendelea kusimamia utekelezaji wa azma yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo viwanda vipya zaidi ya 3,306 vilijengwa katika mikoa mbalimbali ikijumuisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za ujenzi (saruji, marumaru, nondo) na kilimo, hususan, kusindika matunda, mafuta na ngozi. Ujenzi wa viwanda vipya umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 mwaka 2017/18.

(xiv)            Kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma: Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka katika jiji la Dar-es-Salaam kuja hapa katika jiji la Dodoma ambapo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Watumishi wa Umma 6,531 kutoka Wizara zote wamehamia Dodoma. Aidha, inatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais atahamia rasmi Dodoma kabla ya tarehe 31 Desemba 2018.

(xv)            Madini: Sheria za Madini zilifanyiwa mapitio ili kuiwezesha Serikali kunufaika zaidi na rasilimali za madini. Aidha, Serikali ilikamilisha ujenzi wa ukuta wenye mzingo wa km 24.5 kuzunguka migodi ya Tanzanite Mirerani ambao umewezesha kupunguza utoroshwaji wa madini. Juhudi hizi na nyinginezo ziliwezesha kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli yanayotokana na madini kufikia Shilingi bilioni 301.2 mwaka 2017/18 ikilinganishwa na lengo la Shilingi bilioni 194.4.

(xvi)            Elimu: Serikali ya awamu ya tano ilianzisha na imeendelea kutekeleza utaratibu wa kutoa elimumsingi nchini bila ada ambapo Serikali imekuwa ikitoa Shilingi bilioni 20.9 kila mwezi. Juhudi hizi zimechangia ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,078,379 mwaka 2018, na kidato cha kwanza kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 562,695 mwaka 2017.

(xvii)            Usafiri wa Majini: Serikali iliendelea kujenga na kukarabati meli na vivuko katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa Kazi hizi zitarahisisha na kuongeza uwezo wa usafirishaji wa abiria na mizigo. Aidha, uwezo wa meli hizo ni kama ifuatavyo: meli mpya katika ziwa Victoria itabeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo;  ziwa Nyasa abiria 200 na mizigo tani 200; na ziwa Tanganyika abiria 600 na tani 400 za mizigo.

Changamoto za Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti na Hatua za Kukabiliana Nazo

22.             Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2017/18, ni pamoja na zifuatazo:
    (i)            Ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliopo katika sekta isiyo rasmi kwa kuwa hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu;
 (ii)            Kutofikiwa kwa lengo la kodi zinazotokana na ajira (PAYE) kulikosababishwa na kutofikiwa kwa malengo ya ajira mpya na kutoongezeka kwa mishahara kwa wafanyakazi kama ilivyokuwa imetarajiwa. Vile vile, kodi hizi zimeathirika kutokana na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi kwenye migodi ya madini kufuatia kupungua kwa shughuli za uchimbaji madini kwa baadhi ya migodi;
(iii)            kushuka kwa biashara za kimataifa kulikopelekea kutofikia malengo ya uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa imetarajiwa;
(iv)            Upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo kupunguza ufanisi wa utendaji kazi wa Mamlaka;
 (v)            Kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo wakati wa utekelezaji wa bajeti;
(vi)            Changamoto ya masoko na bei ndogo za mazao kwa wakulima; na
(vii)            Kuendelea kuwepo kwa madai mbalimbali yakiwemo ya wakandarasi, watoa huduma, wazabuni na watumishi wa umma.

23.             Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuongeza mapato, Serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwa pamoja na: kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi na utoaji wa elimu kwa walipakodi ili kuongeza mwamko wa kulipa kodi; kuimarisha mifumo na taasisi zinazokusanya mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi na uvujaji wa mapato ya Serikali; kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji wa Sekta Binafsi; na kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kupitia utekelezaji wa Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Corporation Framework - DCF).

MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/20

24.             Mheshimiwa Spika, misingi iliyozingatiwa katika kuweka malengo ya uchumi jumla ni pamoja na: uwepo wa amani, usalama, utulivu na umoja hapa nchini na katika nchi jirani; kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya kiuchumi na kijamii; kutengamaa kwa uchumi wa dunia; utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia; na hali nzuri ya hewa.

25.             Mheshimiwa Spika, Shabaha na Malengo ya Uchumi JumlaShabaha na malengo ya uchumi jumla ambayo yanatokana na takwimu mpya za mwaka wa kizio wa 2015 ni kama ifuatavyo:-
(ii)           Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 5.0 katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22);
(iii)        Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.5 mwaka 2018/19 na wastani wa asilimia 12.9 katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22);
(iv)        Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 21.1 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 na kufikia wastani wa asilimia 20.2 katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22);
(v)           Kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kutoka matarajio ya asilimia 2.9 mwaka 2018/19 hadi wastani wa asilimia 1.1 katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22); na
(vi)        Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.5 katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22).

Mfumo wa Awali wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Kipindi cha Muda wa Kati (2019/20 – 2021/22)

26.             Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kuongezeka hadi Shilingi bilioni 23,206.8 mwaka 2019/20 kutoka Shilingi bilioni 20,894.6 mwaka 2018/19 na kukadiriwa kuongezeka kwa wastani wa asilimia 10.1 katika kipindi cha muda wa kati (2019/20 – 2021/22) hadi Shilingi bilioni 28,113.9 mwaka 2021/22. Mapato ya ndani katika Pato la Taifa yanakadiriwa kuongezeka kutoka asilimia 14.6 mwaka 2019/20 hadi asilimia 14.9 mwaka 2021/22. Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 11.8 hadi Shilingi bilioni 20,124.1 mwaka 2019/20 kutoka Shilingi bilioni 18,000.2 mwaka 2018/19 na kukua kwa wastani wa asilimia 10.1 katika kipindi cha muda wa kati (2019/20 – 2021/22) hadi Shilingi bilioni 24,385.4 mwaka 2021/22. Uwiano wa Mapato ya kodi na Pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kutoka asilimia 12.7 mwaka 2019/20 hadi asilimia 12.9 mwaka 2021/22. Mapato yasiyo ya Kodi (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadariwa kuongezeka hadi Shilingi bilioni 3,082.7 mwaka 2019/20 kutoka Shilingi bilioni 2,894.4 mwaka 2018/19. Aidha, mapato yasiyo ya kodi (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 10.0 na kufikia Shilingi bilioni 3,728.5 mwaka 2021/22.
27.             Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu inatarajiwa kupungua kutoka Shilingi bilioni 3,380.2 mwaka 2019/20 hadi Shilingi  bilioni 3,289.9 mwaka 2021/22. Mikopo kutoka nje na ndani (ikijumuisha Rollover) inatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 6,913.2 mwaka 2019/20 na Shilingi bilioni 6,768.6 mwaka 2021/22.

28.             Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali yanakadiriwa kukua hadi Shilingi bilioni 33,500.2 (asilimia 21.1 ya Pato la Taifa) mwaka 2019/20 kutoka Shilingi bilioni 32,476.0 (asilimia 22.5 ya Pato la Taifa) mwaka 2018/19 na kukadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 6.7 hadi Shilingi bilioni 38,172.5 mwaka 2021/22. Katika mwaka 2019/20, Mishahara (ikijumuisha mishahara ya Taasisi) inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 7,559.0 na kukadiriwa kuongezeka hadi Shilingi bilioni 8,422.7 mwaka 2021/22. Malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje yanakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 8,625.6 mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi Shilingi bilioni 11,023.8 mwaka 2021/22. Kiasi cha kulipia bidhaa, huduma na ruzuku kinakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 4,931.2 mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi Shilingi bilioni 5,166.1 mwaka 2021/22. Matumizi ya Maendeleo yanakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 12,384.4 (asilimia 7.8 ya Pato la Taifa) mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi Shilingi bilioni 13,559.8  mwaka 2021/22.

Maelekezo Mahsusi ya Mwongozo

29.             Mheshimiwa Spika, Maafisa Masuuli wanatakiwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake. Aidha, Kamati za Mipango na Bajeti za kila Fungu zinatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za mwaka 2015. Mwongozo umebainisha masuala muhimu ambayo hayana budi kuzingatiwa na Maafisa Masuuli wakati wa uandaaji wa mipango, bajeti na utekelezaji kama ifuatavyo:
A.                Mahitaji ya Rasilimali Fedha
(i)               Kuhakikisha kuwa makusanyo yote yanawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
(ii)            Kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato;
(iii)         Kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na vile vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21;
(iv)          Kutoingia mikataba yenye vifungu vinavyotoa misamaha ya kodi bila kupata ridhaa ya Waziri wa Fedha na Mipango; na
(v)             Kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kutoa gawio stahiki kwa Serikali.

B.                 Udhibiti Katika Matumizi ya Fedha za Umma
(i)                 Kuhakikisha thamani halisi ya fedha inazingatiwa katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi kwa kuzingatia misingi ya Kanuni za Ununuzi wa Umma kama Force Account, ununuzi wa pamoja na ushindanishwaji wa wazabuni;
(ii)              Kutumia TEHAMA katika mawasiliano Serikalini, kama vile majalada ya kielektroniki kwa lengo la kupunguza gharama na kuongeza ufanisi;
(iii)            Kuhakikisha hati za madai na mikataba ya watoa huduma wa ndani inakuwa katika Shilingi ya Tanzania ili kupunguza athari za mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha;
(iv)            Kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi hasa kwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani;
(v)               Kutenga fedha za kulipa madeni yaliyohakikiwa kwa kutumia Ukomo wa Bajeti uliotolewa; na
(vi)            Taasisi na Mashirika ya Umma yenye uhitaji wa mikopo kuhakikisha zinapata kibali kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134 pamoja na Kifungu cha 60(4) na 62(b) cha Sheria ya Bajeti, SURA 439. Maafisa Masuuli wanaelekezwa kufuatilia kwa ukaribu mikataba yenye dhamana ili kuepuka madeni sanjari.

C.                Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma
(i)                 Kuhakikisha kuwa Taasisi na Mashirika ya Umma yanachangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), (Sura 370), ikijumuisha ziada na itolewe kwa wakati;
(ii)              Kuimarisha ufuatiliaji wa Hisa za Serikali katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache;
(iii)            Kuhakikisha Mashirika ya Umma yanayojiendesha kibiashara yanaandaa Mwongozo wa Gawio utakaotoa utaratibu wa malipo ya gawio kwa Serikali;
(iv)            Kuchambua taarifa za fedha na mwenendo wa Taasisi na Mashirika ya Umma na kupendekeza hatua stahiki za kuboresha, kuunganisha au kuyafuta kwenye Daftari la Msajili wa Hazina; na
(v)               Kufuatilia viwanda na mashamba yaliyobinafsishwa ili kubaini kama yanaendeshwa kuendana na mikataba ya mauzo na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kurejesha Serikalini mashamba na viwanda ambavyo wamiliki watabainika kukiuka mikataba ya mauzo.

30.             Mheshimiwa Spika, maelekezo mahsusi ya Mwongozo yameainishwa kwa kina katika Sura ya Kwanza, Sehemu ya Pili ya Kitabu cha Mwongozo.

MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2019/20

31.             Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 yameainisha maeneo ya kipaumbele yatakayozingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2019/20.  Maeneo hayo yamezingatia  Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 na Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango huo. Maeneo hayo ni:

(i)                Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: Ujenzi wa viwanda ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi (Ruvuma, Mtwara, Kigoma na Bagamoyo); Kukuza kilimo cha mazao, Mifugo na Uvuvi; Maliasili za madini, misitu na wanyamapori; Utalii, Biashara na Masoko; Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa kipekee wa sekta ya kilimo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi, Serikali itaweka msukumo zaidi katika uendelezaji wa sekta hii kwa kutekeleza mikakati na programu mbalimbali hususan ASDP II, uboreshaji wa masoko ya bidhaa za kilimo na uimarishaji wa bei za mazao ya kilimo;

(ii)             Ujenzi wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Kipaumbele kitatolewa kwa miradi ifuatayo: Nishati, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa kufua umeme katika mto Rufiji; Maendeleo ya reli ikijumuisha ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; na Usafiri wa anga ikiwemo kuboresha Shirika la Ndege Tanzania. Aidha, maeneo mengine yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara; madaraja; bandari; usafiri wa majini; teknolojia ya habari na mawasiliano; ardhi na maeneo ya uwekezaji na biashara; huduma za fedha; na ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Vile vile, Serikali itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa katika Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara Nchini wa Mwaka 2010 ikiwa ni pamoja na kusimamia mapendekezo yaliyopo kwenye Blueprint on Policy and Regulatory Reforms;

(iii)           Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Maeneo yatakayopewa kipaumbele ni elimu na ujuzi hususan kusomesha kwa wingi wataalam kwenye fani na ujuzi adimu; afya na ustawi wa jamii; maji na usafi wa mazingira; vijana, ajira na wenye ulemavuhabari, utamaduni, sanaa na michezo; utawala bora na huduma bora kwa wananchi; hifadhi ya mazingira; na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, katika kuimarisha utawala bora ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, Serikali itaendelea kujenga miundombinu wezeshi hususan ofisi, makazi na huduma za jamii katika Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma. Vile vile, msukumo zaidi utawekwa katika kuongeza na kuboresha huduma ya maji; kuunga mkono juhudi za wananchi kukamilisha maboma ya  afya na elimu; na kujenga mazingira ambayo yatawezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye utoaji wa huduma za elimu na afya kama vile upelekaji wa dawa kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drones). Pamoja na hayo, Serikali imeanza kuandaa Muswada wa Sheria ya Maji ambao pamoja na mambo mengine unapendekeza kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini  ili kuongeza kasi ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi;

(iv)           Kuimarisha Usimamizi na Utekelezaji wa Mpango: Miongoni mwa masuala yatakayopewa msukumo ni pamoja na upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kwa riba nafuu, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi, na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.  Maeneo mengine ni yale ya kujenga mazingira wezeshi hususan, kulinda umoja wa kitaifa, ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na ulinzi wa rasilimali za Taifa.

Mikakati ya Kushirikisha Sekta Binafsi kwa Mwaka 2019/20

32.             Mheshimiwa Spika, sekta binafsi inatarajia kuongeza uwekezaji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo hususan katika maeneo ya kipaumbele ikiwemo:-viwanda vya nguo, dawa za binadamu, bidhaa za ngozi, usindikaji wa vyakula, mafuta, ujenzi wa miundombinu wezeshi, huduma za jamii, huduma za fedha, huduma za utalii; na kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda  na maeneo ya teknolojia.

Miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi

33.             Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Maboresho hayo yamepelekea kuundwa kwa miongozo ya kisera, kisheria na kitaasisi ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Kwa msingi huo, miradi ya ubia inayopendekezwa kutekelezwa ni pamoja na: Mradi wa Kusambaza Gesi katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; mradi wa kujenga hosteli za wanafunzi katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) – Dar es Salaam; ujenzi wa vyuo kumi vya Ufundi Stadi; ujenzi waTaasisi ya Taifa ya Saratani; ujenzi wa Reli ya Mtwara – Mbamba Bay kupitia Mchuchuma na Liganga, na Tanga – Arusha – Musoma; na ujenzi wa bandari ya Mwambani Tanga; mradi wa  kufua umeme – Somanga Fungu; uendeshaji wa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam awamu ya kwanza; na ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika mikoa ya Pwani, Mbeya na Mwanza.

34.             Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Maeneo ya Kipaumbele kwa mwaka 2019/20 yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Nne).

HITIMISHO

35.             Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza mwanzoniMaoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge juu ya Mwongozo na Mapendekezo ya Mpango niliyowasilisha yatawezesha kuandaliwa kwa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 ili kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuchochea matokeo yafuatayo: kuongezeka kwa ubora wa huduma za kijamii; kupungua kwa umasikini; kutengamaa kwa viashiria vya kiuchumi na kijamii; na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na biashara. Hivyo, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi na Mashirika ya Umma zinaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wakati wa kuandaa Mpango wa Mwaka 2019/20. Vile vile, Maafisa Masuuli wanatakiwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/20 na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake. Aidha, Kamati za Mipango na Bajeti za kila Fungu zinatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za mwaka 2015.

36.             Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha kwa kuwasisitizia Waheshimiwa Wabunge kwamba katika michango yao wajielekeze zaidi katika kutoa maoni, ushauri na mapendekezo  kwenye miradi na vipaumbele vya Kitaifa badala ya kila mchangiaji kujielekeza zaidi kwenye miradi mahsusi iliyopo jimboni kwake. Ninaamini kuwa kwa kufanya hivyo maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge utaiwezesha Serikali kuandaa Mpango mzuri wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 na Bajeti ya nchi inayojielekeza kutatua kero za wananchi wetu na kuchochea maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania.

37.             Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/20.

38.             Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post