WACHINA WATATU MBARONI KWA TUHUMA ZA RUSHWA SAKATA LA RELI MPYA


Raia watatu wa China wanaofanya kazi na reli mpya nchini Kenya SRG wameshtakiwa kwa kujaribu kuwahonga wachunguzi katika kesi kuhusu utapeli wa mauzo ya tiketi katika mradi wa usafiri wa treni maarufu SGR.

Hii ni baada ya mwendesha mashtaka mkuu nchini Kenya kuidhinisha tume ya kupambana na ufisadi kuwafungulia mashtaka raia hao watatu wa China.

Inaarifiwa takriban $10,000 zinaibiwa kwa siku katika mpango huo, vyombo vya habari vinaripoti.

Mradi huo uliofadhiliwa na unaoendeshwa na serikali ya Uchina wenye thamani ya $3bn ni mradi wenye ukubwa kuidhinishwa nchini tangu Kenya ijinyakulie uhuru mnamo 1963.

Hatahivyo umekabiliwa na kashfa kadhaa tangu kuzinduliwa kwake mnamo Mei 2017.

Li Gen, anayesimamia usafiri, Li Xiaou meneja wa ulinzi na Sun Xin ambaye ni mfanyakazi watafunguliwa mashtaka ya kujaribu kuwahonga maafisa waliokuwa wanachunguza sakata ya wizi wa pesa zinazotokana na mauzo ya tiketi.

Watatu hao wanaripotiwa kujaribu kuwahonga maafisa wa uchunguzi shilingi 500,000 za Kenya au dola 5,000.

Ukizungumzia suala hilo ubalozi wa China mjini Nairobi kupitia mkurugenzi wake wa mawasiliano Zhang Gang alisema Ubalozi unaheshimu uchunguzi unaofanywa na mamlaka za Kenya kuambatana na sheria za Kenya.

Walifishwa katika mahakama katika mji wa pwani Mombasa na jaji ameamuru wasalie rumande mpaka ombi lao la kuachiwa kwa dhaman litakaposikizwa Novemba 30.

Inadaiwa mpango huo umehusisha kukusanywa kwa fedha za malipo ya tiketi zilizorudishwa na kuelekezwa kwingine, kwa mujibu wa ripoti katika gazeti la Daily Nation.

Watatu hao hufanya kazi na kampuni ya China Roads and Bridge Corporation (CRBC) katika kituo cha treni mjini Mombasa.

Chanzo: Bbc

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527