KIDATO CHA PILI KUANZA MTIHANI WA UPIMAJI KITAIFA KESHO

Watahiniwa 544,866 wa shule za sekondari 4,725 wamesajiliwa kufanya mtihani wa upimaji wa kitaifa kidato cha pili kuanzia kesho Novemba 12 hadi 23, kati yao asilimia 47.93 ni wavulana na wasichana ni asilimia 52.07.


Pia kuanzia Novemba 22 hadi 23 watahiniwa 1,358,217 kutoka shule za msingi 17,336 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya upimaji darasa la nne kati yao wavulana ni 682,193 (asilimia 50.23) na wasichana ni 676.024 (asilimia 49.77).


Akizungumza na waandishi wa habari leo Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amesema kumekuwa na ongezeko la watahiniwa kwa asilimia 4.41 kwa kidato cha pili na ongezeko la asilimia 13.57 kwa darasa la nne.


"Mwaka 2017 kidato cha pili kulikuwa na watahiniwa 521,855 na darasa la nne walikuwa 1,195,970 hivyo tunaweza kuona ongezeko la watahiniwa 185,258 kwa ujumla," amesema Dk Msonde.


Amesema katika watahiniwa wa kidato cha pili walio na mahitaji maalumu wapo 775 ambapo kati yao 411 ni wenye uoni hafifu, wasioona 66, wenye ulemavu wa kusikia 256 na 36 ni walio na ulemavu wa viungo.


Kwa watahiniwa wa darasa la nne walio na mahitaji maalumu wapo 3,336 kati yao wenye uoni hafifu ni 120, wasioona 120, wenye ulemavu wa kusikia 725 na 1,776 ni walemavu wa viungo vya mwili," amesema Dk Msonde.


Dk Msonde pia amewataka wamiliki wa shule za binafsi kuepuka kuingilia majukumu ya wasimamizi huku akibainisha kuwa baraza halitasita kukifutIa mtihani kituo kitakachobainika kufanya udanganyifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post