NONDO : SITARUDI NYUMA KUTETEA HAKI ZA WANAFUNZI

Baada ya kuachiwa huru   na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, ameeleza magumu aliyopitia wakati akitetea wanafunzi huku akiwa anaendelea na kesi yake ya kudaiwa kujiteka.

Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 ilitolewa jana na  Hakimu Mfawidhi, Liad Chemshana wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.

Katika kesi hiyo  ilidaiwa kwamba Machi 7 mwaka huu akiwa Ubungo Dar es Salaam, Nondo  alichapisha taarifa hizo akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya jamii.

Akizungumza nje ya mahakama  baada ya hukumu hiyo, Nondo  alisema katika kipindi chote wakati anatetea haki za wanafunzi   na kuendelea na kesi dhidi yake, alipita kwenye nyakati nzito katika  maisha yake ila anamshukuru Mungu kwa vile  Mahakama imetenda haki.

Alisema pamoja na hali hiyo, kamwe hatorudi nyuma katika mapambano ya kutetea haki za wanafunzi nchini kwa kupaza sauti   mambo yanapopindishwa.

“Katika  kipindi  chote  ambacho  nilikuwa napitia mapito  haya  mazito  iwapo  ningekuwa sina  msimamo ningekuwa  nimerudi  nyuma na kukata  tamaa kukubali  kila  nilichoshinikizwa  niseme  niweze kuachiwa.

“…  lakini  sikuwa  tayari kwa hilo nilimtanguliza Mungu  ambaye leo (jana),  ameweza  kunipigania, namshukuru Mungu na Mahakama kwa kutenda haki.

“Pia naushukuru Mtandao wa  Watetezi wa  Haki za Binadamu (THRDC),  muda wote wamekuwa nami, asanteni sana mawakili wangu, asanteni Watanzania wote sitorudi nyuma kuwa mtetezi wa wanyonge,” alisema Nondo.

Alisema amepita  katika mapito mazito kwa ajili ya kupigania  haki za  wanafunzi na kamwe hataacha kuendeleza harakati za kupigania haki zao.

“Mungu ni mwema ametenda mema juu yangu na sitarudi nyuma, nawaombeni niwashukuru pia waandishi wa habari  nchini hasa Iringa ambao muda wote mlifika kufuatilia  kesi  yangu naomba leo (jana)  niishie hapa.

“Nitasema zaidi ila leo (jana) sipo vizuri nina furaha kubwa,” alisema Nondo huku akibubujikwa machozi

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema  Mahakama imeweza kutenda haki na uamuzi uliotolewa na mahakama hauna hata chembe moja ya upendeleo .

Katika  kasi hiyo, Nondo alikuwa  akitetewa na mawakili   wawili, Chance Luoga na Jebra Kambole  ambao walieleza imani kubwa  kwa mahakama kupitia hukumu hiyo.

Wakili Kambole alisema kuna uonevu mkubwa ambao  polisi walionyesha kumtendea mteja wao ambao mahakama  pia  imeuona.

Hukumu  hiyo  ilichukua    saa moja  kusomwa  huku  askari  wa  Kikosi cha  Kutuliza  Ghasia  (FFU)  wakiwa  wametanda nje ya mahakama  hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post