MWAKYEMBE AZUNGUMZIA ' TAIFA STARS KUZITAPIKA MIL 50 ZA JPM'

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyemba amesema akifika Tanzania atamueleza Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwa kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Lesotho kuwa ni bahati mbaya na kumuahidi kuwa kwenye mechi dhidi ya Uganda Taifa Stars itaibuka na ushindi.

Kauli hiyo ya Dkt Mwakyembe imekuja saa chache baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya timu ya Lesotho ambapo Taifa Stars ilifungwa bao 1-0.

Akizungumza na waandishi wa habari Nchini Lesotho Waziri Mwakyembe amesema “alisema turudi na ushindi, nitamwambia tumefungwa moja na tunasubiri mechi ya Uganda ambayo lazima tushinde, huu ndiyo moyo wa kimchezo, ukijikunyata utakuwa unadundwa ngumi kila wakati”

“Milioni 50 tulizopewa zimetusaidia kufungwa bao moja tu pengine tungefungwa hata sita ila tumefungwa sawa ndiyo mchezo tunaendelea kutafuta ushindi, tumejitahidi sana ila kwa sasa sio kichwa cha mwendawazimu tena,” ameongeza Mwakyembe.

Jana Rais Magufuli alieleza kuufatilia mchezo baina ya timu ya Taifa dhidi ya Lesotho, katika mtandao wa Twitter aliandika "vijana wangu Taifa Stars, muda mfupi ujao nitakuwa nikitazama mchezo kati yenu na timu ya taifa ya Lesotho, mimi na Watanzania wenzangu tunawatakia mchezo mwema, mrudi na ushindi,".

Akizungumza wakati akikutana na kikosi hicho cha timu ya Taifa Ikulu jijini Dar es salaam oktoba 19 Rais Magufuli alisema “nawapa hela hizi za walipakodi zikalete ushindi na mkifungwa mtazipika kwa njia nyingine”.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post