MBAO ZA MAGENDO ZAKAMATWA ZIKISAFIRISHWA KWA TRENI SHINYANGA

Shehena ya mbao imekamatwa katika stesheni ya Shinyanga ikisafirishwa kimagendo katika treni ya mizigo kutoka mkoani Tabora kuelekea Mwanza.

Shehena hiyo imekamatwa baada ya kuwekwa mtego na wakala wa huduma za misitu wakishirikiana na Jeshi la Polisi.

Akizungumza jana Ijumaa Novemba 23, 2018 ofisa misitu Wilaya ya Kahama mkoani humo, Mohamed Dossa alisema mbao hizo zimekamatwa wakati mabehewa hayo yakiwa katika kituo cha bandari kavu cha Isaka.

Alisema baada ya kupata wasiwasi waliwasiliana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) mkoani humo pamoja na polisi na kufanikiwa kukamata mabehewa mawili yakiwa na mbao hizo.

Treni hiyo ya mizigo baada ya kukaguliwa mabehewa mawili yalibainika kuwa na shehena ya mazao ya misitu ikiwemo mbao, asali na milango.

Alisema vitu hivyo huenda vimevunwa na kusafirishwa kinyume cha sheria, bila kulipiwa ushuru wa Serikali.

Alisema kukamatwa kwa mabehewa hayo kulitokana na taarifa zilizotolewa na wasamaria wema wa wakala wa misitu mkoani Tabora na hivyo treni hiyo kuzuiwa baada ya kufika mjini Shinyanga.

“Treni hiyo ya mizigo ilikuwa ikitoka mkoa wa Tabora, walianza kuishtukia katika kituo cha bandari kavu cha Isaka na askari wa TFS aliyejulikana kwa jina la Leonard Maguta alipopanda katika treni hiyo kufuatilia alipigwa na askari waliokuwemo ndani na kushushwa njiani,” alisema Dossa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule akizungumza na waandishi wa habari alisema katika tukio hilo wanawashikilia watu wanne ambao majina yao yamehifadhiwa hadi uchunguzi utakapokamilika.

Alisema mbao zilizokamatwa ni zile ambazo haziruhusiwi kuvunwa mpaka kwa kibali maalumu na zilikuwa zikisafirishwa bila kuwa na kibali.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewataka watumishi kuwa waadilifu na kuacha kusafirisha vitu haramu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi na kuwataka kufuata taratibu na sheria.

“Usafirishaji wa magendo kwa njia ya reli umekithiri sana na mizigo mingi ya aina hiyo imebainika na kukamatwa ambapo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa wanapoona hali kama hiyo ili kuchukua hatua kabla ya tukio kumalizika kutendeka” alisema mkuu wa wilaya .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post