DC ILEMELA : TUMIENI MABARAZA YA WAZEE KUISHAURI SERIKALI

Wazee wa Ilemela pamoja na wazee wote nchini, wametakiwa kuyatumia mabaraza yao yaliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria kuishauri Serikali katika kutekeleza mambo ya msingi ya kujiletea maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza Mhe. Severine Lalika wakati akizindua Baraza la Wazee la Wilaya ya Ilemela, ambapo amewataka wazee hao kuwa sehemu ya serikali sanjari na kuwa mwarobaini katika kufichua na kutafuta suluhu ya changamoto zote zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato na mmomonyoko wa maadili.


"Nyie ni wadau wa maendeleo hivyo mnao wajibu wa kuishauri Serikali katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za kisiasa, kijamii na uchumi,"Alisisitiza.


Aidha amewapongeza viongozi wote waliochaguliwa kuongoza baraza hilo sambamba na kuwahakikishia ushirikiano huku akiahidi kukutana nao tena haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kujadiliana kwa pamoja juu ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.


Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Ndugu Said Kitinga alisema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa na desturi ya kukutana na wazee na kubadilisha nao mawazo juu ya mambo mbalimbali ya kijamii katika awamu zote za uongozi tangu kupata uhuru mpaka awamu ya sasa hatua inayodhihiridha juu ya umuhimu wa kundi hilo katika jamii.


Kwa upande wake mratibu wa baraza la wazee wilaya ya Ilemela Bi Neema Kavishe ametaja umuhimu wa kuanzishwa kwa baraza hilo ikiwemo kutumika na Serikali, wasiasa, watendaji na taasisi kama chanzo cha habari na sehemu sahihi ya kupata takwimu za wazee kabla ya kupanga mipango ya kimaendeleo inayohusu wazee.


Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Ilemela Shehe Mohamed Yusuph, mbali na kuupongeza uongozi wa wilaya ya Ilemela kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wazee hao, ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Daktari John Pombe Magufuli kwa kulithamini kundi hilo katika jamii na kuamua kuanzisha utaratibu wa kupata matibabu ya huduma za afya bila malipo kwa kutumia kadi maalumu huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza shughuli za kimaendeleo.


Baraza la Wazee la Wilaya ya Ilemela liliundwa mnamo tarehe 22/09/2018 ambapo Shehe Mohamed Yusuph Hasan alichaguliwa kuwa Mwenyekiti huku , Makamu Mwenyekiti akiwa Bibi. Prisca Mwisijo, Katibu Ndibai Yukao, Katibu Msaidizi Jackson Kabote, Mweka Hazina Ndugu Daniel Makorere pamoja na wajumbe wawili wakiwakilisha upande wa wanaume na wanawake ambao ni Bwana Saulo Mihigo na Bibi Mary Masalu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527