WANAJESHI WAZINDUA KONDOMU ZAO,ZIMEANDIKWA ULINZI ' USIENDE NYAMA KWA NYAMA'

Jeshi la Uganda limezindua nembo mpya ya mipira ya kondomu ambayo inalenga kutumiwa na wanajeshi nchini humo.

Kondomu hizo zimepewa jina Ulinzi na zinatarajiwa kusaidia katika juhudi za kupunguza kuenea kwa virusi vinavyosababisha Ukimwi.

Kitengo cha kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi jeshini kilizindua nembo hiyo mpya kwa ushirikiano na mashirika mawili yasiyo ya kiserikali, Population Services International (PSI) - Uganda na Pace Uganda.

Kwenye pakiti za kondomu hizo, pameandikwa 'Usiende Nyama kwa Nyama', kuwahamasisha wanajeshi kutumia kinga wanaposhiriki tendo la ndoa.

Mkuu wa majeshi ya ardhini Uganda Brigedia Leopold Kyanda ndiye aliyeongoza uzinduzi wa kondomu hizo ambapo alitoa wito kwa wanajeshi kuhakikisha wanajilinda na kujikinga. Ni kwa njia hiyo pekee, alisema, ndipo wanaweza kulilinda taifa.

"Iwapo mwanajeshi binafsi hatahakikisha kwamba yuko salama, basi hawezi kuilinda nchi yake na ndio maana kama jeshi tumechukua njia hii, kuhakikisha kwamba mko salama kisha muweze kuilinda nchi," alisema Brigedia Kyanda.

Mwakilishi wa Pace Uganda alisema ni kawaida kwa wanajeshi wakiwa kazini kukutana na kufanya tendo la ndoa na wanawake, na hivyo akasisitiza kwamba ni muhimu kuwalinda wake zao wanaporejea nyumbani.

Mkurugenzi wa PSI nchini Uganda Dkt Dorothy Baraba alisema kwa sasa kondomu hizo ni za wanaume pekee lakini karibuni watawashirikisha wanawake.

Alisema mpango huo umetokana na agizo la afisi ya rais na kwamba wanautekeleza kama washirika wa UPDF.Jeshi la Uganda pia huuza maji ya chupa yajulikanayo kama Uzima

Si mara ya kwanza kwa jeshi la Uganda kushiriki katika kuendeleza na kusambaza bidhaa Uganda.

Mwaka 2015, walizindua nembo ya maji ya chupa kwa jina Uzima kwa lengo la kuimarisha maisha ya wanajeshi kupitia kuwapa mapato.

Maji hayo huuzwa madukani na pia hutumiwa sana katika shughuli rasmi za serikali.

Maji hayo huandaliwa na kampuni ya jeshi ya NEC Uzima Ltd ambayo huhudumu chini ya Shirika la Biashara la Taifa (NEC).
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527