BAADA YA KOROSHO, SERIKALI YAHAMISHIA MSULI KWENYE MAHINDI

Baada ya Serikali kununua korosho zote kwa wakulima mikoa ya Kusini, Lindi, Mtwara na Ruvuma, imeanza kushughulikia zao la mahindi katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe na Mbeya.


Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa mahindi Afrika Mashariki katika mikoa tajwa, lakini imeelezwa mahindi hayo kwa kiasi kikubwa yamekosa soko baada ya lile la ndani kujitosheleza kwa chakula.


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akiongea na gazeti la Serikali laHabarileo jana, alisema serikali imeshatuma timu ya wataalamu wake mikoa hiyo ili kutathmini kiasi cha mahindi kilichopo na wakati huo huo kuna timu ya wataalamu inayoendelea kufanya tathmini ya masoko ya zao hilo kwa nchi jirani ili kusaidia upatikanaji wa masoko.


Alisema nchi zilizoonesha nia ya kutaka kununua mahindi kutoka Tanzania ni pamoja na Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini pia serikali inawatumia mabalozi wake walioko nchi jirani kama vile Kenya na Sudan Kusini kufuatilia kama nako wanaweza kupata soko la mahindi hayo.


“Timu tuliyounda inajumuisha wataalamu kutoka taasisi za Serikali, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko; tumewapa wiki moja na nusu watueleze tuna tani ngapi za mahindi nchini,”alieleza Waziri Hasunga.


Alisema hivi sasa kuna ziada ya mazao ya chakula ya asilimia 123 na lengo la serikali ni kuliongezea thamani zao la mahindi kabla ya kuyauza nje kupata pato zuri zaidi lakini kutokana na uhaba wa viwanda au mashine ya kuliongezea thamani, kuna baadhi ya nchi yatauzwa mahindi na nyingine utauzwa unga.


Kwa upande wa Mbunge wa Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, Daimu Mpakate, alisema kuwa ni vyema serikali ikalitumia vyema soko la mahindi Malawi kwa kuitumia Bodi ya Mazao Mchanganyiko.


Alisema Ruvuma ina zaidi ya tani milioni 1.5 za mahindi, lakini Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), uwezo wao wa kununua mahindi hayo siyo zaidi ya tani 30,000 hivyo kuhitaji kusaidiwa.


Alisema kwa kuwa NFRA wananunua mahindi kwa hifadhi ya taifa na siyo kwa ajili ya biashara kama bodi nyingine, ni vyema serikali ikaiongezea uwezo Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua mahindi ya wakulima na ikiwezekana wayaongezee thamani kwa kutengeneza unga na kisha kuuza nchini Malawi.


Alisema ingawa NFRA wananunua mahindi kwa Sh 500 kwa kilo, kutokana na uwezo mdogo wa kifedha , wakulima wanalazimika kuuza kwa wanunuzi binafsi kwa wastani wa Sh 200-270 kwa kilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527