Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amewasimamisha kazi watumishi watatu wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Jiji la Arusha, kwa tuhuma ya kushirikiana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo ambalo linaongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Lukuvi alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha jana kufuatia kuwepo tuhuma nyingi za matapeli ya viwanja kushirikiana na baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali wa viwanja.
Maafisa ardhi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo za kushirikiana na matapeli kudhulumu viwanja kwa wamiliki halali katika jiji la Arusha ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.
Mbali na kusimamishwa kazi kwa watumishi, Waziri Lukuvi, aliagiza maafisa Ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao wasipatiwe huduma katika masuala yoyote ya ardhi kufuatia kuonekana kujihusisha na mipango ya utapeli wa viwanja kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha.
Kufuatia kadhia hiyo, Lukuvi ameagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa Mahakama nchini, kusainiwa na Afisa Ardhi Mteule au Msajili wa Hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima afahamishwe uwepo wa kesi husika.
"Kuanzia sasa 'summons' zote zipokelewe na Maafisa Ardhi Wateule, Makamishna au Wasajili wa Hati wa Kanda na watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha" alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema matapeli wa viwanja wamekuwa wakifungua kesi katika Mabaraza ya Ardhi dhidi ya wamiliki halali na wakati mwingine matapeli hao hawawafahamu hata wamiliki lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda mrefu hasa ikizingatiwa baadhi ya wamiliki hawana uwezo wa kuweka mawakili na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.
Via>>EATV