VIJANA 7 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUHARIBU NOTI ZA SH 70,000

Vijana saba wenye umri kati ya miaka 21 na 24 leo Jumanne Oktoba 2, 2018 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kuharibu noti za Sh70,000.


Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono amewasomea mashtaka yao leo, akieleza kuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 299 ya 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hamza Wanjah.


Kombakono amewataja washtakiwa hao kuwa ni Vicent Kaduma (24), Rogers Swale (23), mwanafunzi Doreen Mwenisongole (22), Kelvin Mgeyekwa (23), Elia Chengula (24), Said Sadiq (21) na Ramadhani Selemani (23) wote wakazi wa Dar es Salaam maeneo ya Bahari Beach na Kunduchi.


Kombakono amedai Septemba 16, 2018 jijini Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka washtakiwa hao waliharibu kwa kuzikanyaga noti za Sh 70,000 za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.


Wakili wa upande wa utetezi, Stoki Joackim anayewatetea washtakiwa wote aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake kwa sababu shtaka linalowakabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria na kwamba dhamana ni haki ya washtakiwa.


Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Wanjah alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa kwa kumtaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua na nakala za kitambulisho na kwamba kila mdhamini asaini bondi ya Sh 2 milioni.


Washtakiwa wote walifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 2, 2018 itakapotajwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post