Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kumuondoa mara moja katika nafasi yake Mkuu wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), Paschal Highmagway kutokana na kutoa taarifa ya uongo ya kumsifia mkandarasi ambaye ameshindwa kukamilisha ujenzi.
Agizo hilo alilitoa jana Oktoba 5, 2018 alipotembelea chuo hicho na kukagua ujenzi wa majengo mbalimbali pamoja na ukarabati unaofanywa na wakandarasi wawili tofauti ambao ni Kampuni ya Masasi iliyokwisha kamilisha kazi na mkandarasi Afriq Engeneering yenye makao yake jijini Dar es salaam ambayo haijakamilisha.
Profesa Ndalichako alisikitishwa na taarifa aliyoitoa mkuu wa chuo hicho akionyesha wazi kumsifia mkandarasi Afriq Engeneering kwa kazi nzuri, ambaye tangu apewe mkataba Agosti 22 mwaka 2016 hakuna hata jengo alilokamilisha huku mkataba wake ulikuwa unamalizika Aprili 5, 2018 huku Serikali ilimuongezea muda hadi Septemba 15, 2018.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Ndalichako amemuomba Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Diwani Athuman kutuma wataalamu wake kwenda kuchunguza ujenzi wa mradi huo unaofanywa na Afriq Engeneering unaoonyesha dalili za wazi za kutawaliwa na vitendo vya rushwa.
“Nitamuomba mkurugenzi mkuu wa Takukuru nchini (Diwani) kuanza kuchunguza mradi huu wa Shinyanga pia maofisa wa wizara yangu waliohusika kusimamia mradi huu nao wachunguzwe,” alisema
“Haiwezekani huyu mkandarasi ameshapewa onyo halafu wamesikia nakuja huku Oktoba 2, 2018 wakamlipa Sh244.8 milioni kitendo hicho kimenisikitisha sana,” aliongeza
Alisema wale wote waliotumia fedha hizo kinyume na maelekezo watazitapika huku akionyesha kushangaa na kusikitishwa kitendo cha mkuu wa chuo kumsifia mkandarasi ambaye ameharibu kazi.
“Mradi huu ninakuagiza mkandarasi AFRIQ Engeneering kukamilisha majengo yote ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa ufanye kazi usiku na mchana maana Serikali imetumia Sh9.4 bilioni kwenye ujenzi huo na mkandarasi ambaye hajakamilisha kazi tayari ameshalipwa Sh2.7 bilioni,” amesema.