IKULU YASEMA HABARI YA MAGUFULI KUWATAKA WANAUME KUOA WANAWAKE WAWILI NI UHALIFU WA MTANDAO

Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, imekanusha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinazodai kuwa Rais Dk. John Magufuli amewataka wanaume nchini kuoa wanawake zaidi ya mmoja kutokana na wingi wao ili kupunguza vitendo vya ukahaba.


Kauli hiyo ya Ikulu imekuja baada ya taarifa zilizowekwa kwenye tovuti ya nipasheonline.com inayodaiwa kusajiliwa nchini Kenya na zaidi ikiwa haina uhusiano wowote na gazeti la Nipashe kusambaa kwa kasi na hivyo kuzua mjadala ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Taarifa hizo tayari zimeonekana kuishtua Ikulu ambapo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Msemaji huyo wa Rais Magufuli, Msigwa aliandika huku akiwa ameambatanisha na picha ya habari hiyo kuwa; “Ni uzushi  na uhalifu wa mtandao ,Mhe. Rais hajawahi kuzungumzia jambo hili mahali popote, puuzeni.”
Mtandao huo ulidai kuwa Rais Magufuli alitoa kauli hiyo katika mkutano wa wanaume 14,000 ambao walipokea mafunzo katika nyanja tofauti jijini Dar es Salaam.

Mtandao huo umeandika kuwa kuna idadi kubwa ya wanawake nchini na kulingana naye kuna wanawake milioni 40 na wanaume milioni 30.

“Siwalazimishi, lakini ninawashauri kuoa wake wawili au zaidi ili kupunguza idadi ya wanawake wasio na waume,” uliandika mtandao huo  na kudai kuwa ni kauli ya Dk. Magufuli.

Taarifa za mtandao huo ambazo zimesambaa maeneo mbalimbali ndani ya na nje ya bara la Afrika  zimeonekana kuibua mjadala mzito.

Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka ni miongoni mwa walioibuka na kujadili suala hilo.

Mama Tibaijuka kupitia andiko lake alilolituma katika mitandao ya kijamii, licha ya kuonyesha wasiwasi kuhusu ukweli wa taarifa hiyo, alichambua kwa kutumia namba ambazo zilionyesha kuwa ni jambo lisilowezekana kwa wanaume wote wa Watanzania kuoa wake wawili kila mmoja.

“Nijuavyo mimi Mhe Rais wetu Magufuli ni mcheshi sana, huwa anapenda kutania, lakini wengine labda tunamiss  huo utani, sasa hizi habari eti kasema kuna uwezekano wa kila mwanaume Mtanzania kuoa wanawake wawili wawili eti kwa kuwa ni wengi kwa nini magazeti yetu kama (analitaja gazeti lililonukuliwa kudaiwa kuandika kauli hiyo) yanauchukulia literally kama ni kweli kasema hivyo?

“Niko Marekani, sijaona hiyo audio clip ya Rais, ila naona anakuwa quoted out of context, kiuhalisia  haiwezekani kuwa na wanawake wawili wawili, hakuna wanawake wengi namna hiyo kwa kuzaliwa ni hamsini kwa hamsini.

Tofauti ni ndogo, tunasema “it is not statistical significant”. Mungu anabalansi jinsia zote,” aliandika Profesa Tibaijuka.

Alisema katika sensa ya mwisho ni ya 2012 ilibaini kwamba  Tanzania ilikuwa na watu 44,928,923 ambapo kati ya hao wanaume walikuwa 21,869,990 na wanawake 23,058,933.

Alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa, ongezeko la watu kwa kila mwaka ni asilimia 2.7%. Kwa hiyo mwaka 2018 Tanzania inakadiriwa kuwa na wanaume 23,066,912 na wanawake 27,786,401. Jumla 50,853,314.

“Je, kuna wanawake wangapi kwa kila mwanaume kwa sasa? Unachukua milioni 27 unagawa kwa milioni 23 unapata 1.204…. kwa hiyo hakuna uwezekano wa kila mwanamume kuoa wake wawili wakatosha,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alisisitiza kuwa, kwa maana hiyo, sera ya wake wawili wawili haitekelezeki, kwani hakuna wanawake wa kutosha na namba hazikubali.

Alisema taarifa  inayosambaa kwamba  wanawake wanaonekana ni wengi kuliko wanaume zinatokana na sababu za kijamii na kiuchumi.

Alisema wanaume wana hali ngumu zaidi kuliko wanawake kutokana na wengi wao wamefungwa, wamelowea wanatumia madawa ya kulevya, hawana kazi, wakati jamii ikiwataka wanawake kuolewa na mtu mwenye uwezo.

“Kwa hiyo ni wanaume wanasakamwa zaidi na tatizo la umaskini, wanaume wengi wanashindwa kumudu familia na kuzitunza, kwa hiyo ama hawaoi au wanatelekeza familia zao, kwa hiyo ukiangalia unakuta wanaume wapo, lakini wengi hawana uwezo wa kuoa, wazungu wanasema “eligible bachelors”, aliandika Profesa Tibaijuka.

Profesa Tibaijuka aliwataka watu wanaopenda kufahamu kuhusu utafiti huo wasome machapisho yake kwenye jarida maarufu la ‘Journal of World Development Vol 25 No 6’ lililochapishwa na Pergamon Press of the American University Juni 1997.

Alisema ndoa ya wake wengi haifai, kwakuwa itawatesa wanaume, wengine watakosa wake, pia itachochea umalaya badala ya kuupunguza.

Profesa Tibaijuka aliendelea kuhoji suala hilo kwakutolea mfano wa nchi ya China walipokuwa na sera ya mtoto mmoja mmoja.

“Kwa kuwa wanaume ndio wanapendwa wazazi wengine waliwaua watoto wa kike kusudi wapate wa kiume wanaopendelewa, kwa hiyo China kuna uhaba mkubwa wa wanawake hadi wanatekwa nyara hata wale walioolewa na kupelekwa vijijini,” aliandika Profesa Tibaijuka.

Alimaliza kwakushauri sera ya hamsini kwa hamsini  na mume mmoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post