POLISI DODOMA WANASA LORI LIKIWA NA POMBE KALI NA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU

Mnamo tarehe 05.10.2018 majira ya saa 14:00 mchana huko maeneo ya Igawa, Kata ya Lugerele, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya
Mbeya-Iringa, Jeshi la Polisi likiwa katika Doria katika Barabara hiyo, askari walilitilia mashaka Gari lenye namba za usajili T.233 CXL aina ya IVECO likiwa na Tela lenye namba T.574 CNC Mali ya Kampuni ya OIL COM likiwa linaendeshwa na Dereva MICHAEL GODSON likitokea Zambia kuelekea Dar es Salaam na baada ya kulisimamisha na kufanya upekuzi katika gari hilo walikuta vipodozi vya aina mbalimba katoni 15 na katoni 02 za pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya Officer zikiwa zimefichwa kwenye tool box.


Vipodozi hivyo vilivyokamatwa ni:-
Dermotyl Lotion 30mls box mbili zikiwa na chupa 600
Dermotyl Cream 30gm box mbili zikiwa kwenye tube 600
Dermaclair Lotion 30mls box mbili zikiwa na chupa 600
Dermasol Pro-Active Cream 30gm box mbili zikiwa kwenye tube 600
Dermo-Gel 30gm box mbili zikiwa na kwenye tube 600
Perfect White Cream 150mls box nne zikiwa na chupa 192
Neoprosone –Gel 30gm box moja lenye tube 300
Pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina officers cane spirit 200ml chupa 20 na officers Verve Alco Energy Drink 200mls chupa 18.


Aidha Dereva wa gari hilo mara baada ya kusimamishwa na askari aliacha gari na kukimbia. Msako mkali wa kumtafuta unaendelea.


KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo tarehe 07.10.2018 majira ya saa 00:30 usiku huko Katika kijiji cha Mwaoga, Kata ya Makongolosi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wanyamapori wakiwa katika msako wa pamoja waliwakamta 1. PAUL PASPEL MWANIWITI [40] na 2. MWANDU SIMBILIGWI [38] wote wakazi wa Mwaoga Wilaya ya Chunya wakiwa na mnyamapori aina ya kakakuona ambaye thamani yake ni Usd 950 bila kibali. Upelelezi unaendelea.


KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo tarehe 05.10.2018 majira ya saa 06:00 asubuhi Huko kitongoji cha Kisungu, kijiji cha Upendo, Kata ya Upendo, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na askari wa Wanyamapori wakiwa katika Msako wa pamoja walimkamata HELENA IKUBI [36] Mganga wa kienyeji/asili na Mkazi wa Kijiji cha Kisungu akiwa na nyara za Serikali ngozi moja ya Chui, Ngozi moja ya Nguchilo, mkia wa Nyumbu, ngozi ya Nyegere, kipande cha ngozi ya Nyati, pamoja na kipande cha ngozi ya Simba bila kibali. Upeleleezi unaendelea.


Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi wa mashauri haya kukamilika.


KUPATIKANA NA SILAHA {GOBOLE}
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja aitwaye SUZANA JULIUS @ MBENYA [28] Mkazi wa Itumbi Wilaya ya Chunya akiwa na silaha aina ya Gobole na risasi 10 za goroli pamoja na baruti.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.10.2018 majira ya saa 13:15 mchana katika msako uliofanyika huko Kitongoji cha Itumbi, Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa alikuwa ameificha silaha hiyo kwenye nyasi nyuma ya nyumba yake na risasi alikuwa amezificha juu ya paa la nyumba hiyo. Upelelezi unaendelea.


KUPATIKANA NA VIFAA VYA KUTENGENEZEA SILAHA {GOBOLE}
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja aitwaye MWITA WHATSON @ SHEGA [38] Mkazi wa Itumbi Wilaya ya Chunya akiwa na vifaa vya kutengenezea Silaha aina ya Gobole.


Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.10.2018 majira ya saa 12:30 mchana katika msako uliofanyika huko Kitongoji cha Itumbi, Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Vifaa alivyokamatwa navyo ni:-
Cocking handle,
Trigger,
Trigger guard,
Mtutu na mdeki.
Vifaa hivyo vilikuwa vimefukiwa shambani kwake. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.


JALADA LA UCHUNGUZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye ASHA SIELI [35] Mkazi wa Iwanga Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa kosa la kumvamia usiku EVA AMONI [35] Mkazi wa Iwanga akiwa amelala nyumbani kwake kwa nia ya kutenda kosa.


Tukio hili limetokea mnamo tarehe 05.10.2018 majira ya saa 00:00 usiku huko Iwanga, Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini ambapo EVA AMONI akiwa amelala katika nyumba yake anayoishi na watoto wake wawili alivamiwa na watu wawili mmoja mwanamke [amekamatwa] na mwingine mwanaume ambaye baada ya kuingia ndani alimkaba mhanga shingoni lakini alifanikiwa kuomba msaada kwa majirani na watuhumiwa walikimbia.


Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata ASHA SIELI ambaye ni shangazi wa mhanga wa tukio hilo baada ya kutambulika kwa sauti na mlalamikaji. Aidha msako mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa mwingine aliyefahamika kwa jina la JUMA HORONGO ambaye alikimbia mara baada ya tukio hilo. Upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hili unaendelea ili kubaini kiini cha tukio kwani mhanga ana watoto wawili ambao ni walemavu wa ngozi @ albino.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na Operesheni, Misako na Doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa ili kuimarisha ulinzi na usalama. 


Aidha Operesheni za usalama barabarani zinaendelea katika barabara kuu hasa katika maeneo ya Mlima Iwambi, Igawilo, Nyoka na Mwansekwa katika utaratibu wa kupitisha malori na magari madogo na ya abiria kwa awamu tofauti ili kuepuka madhara makubwa pindi ajali inapotokea. 


Pia zoezi la ukaguzi wa magari, ukaguzi na uhakiki wa leseni za madereva, kuwapima ulevi madereva pamoja na kudhibiti mwendo kasi linaendelea katika maeneo yote ya Mkoa wa Mbeya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post