MWINYI AJITABIRIA KIFO 'SINA SIKU NYINGI ZA KUIACHA DUNIA'


Hotuba aliyoitoa rais wa zamani, Ali Hassan Mwinyi jana Ikulu jijini Dar es Salam, akidokeza muda wake uliosalia duniani, ilimtoa machozi waziri wa zamani, Mwantumu Mahiza.

Mwinyi, ambaye ni mdhamini wa Skauti, alitoa hotuba hiyo wakati wa hafla ya kuapisha wateule wa Rais, akiwemo Mahiza, ambaye amekuwa Skauti Mkuu.

Ukumbi wa mkutano ulikuwa kimya wakati Mwinyi alipotamka maneno hayo, akionekana kutoa wosia kwa wateule kulinda heshima yake.

“Sina siku nyingi za kuiacha dunia,” alisema rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Pili na maneno hayo yalimfanya Mahiza ainamishe kichwa na kuonekana akijifuta machozi.

“Leo nina miaka karibu 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia. Sitaki niende huko ninakokwenda na aibu nyuma yangu,” alisema Mwinyi.

Kiongozi huyo mstaafu alitoa mfano wa kisa kimoja cha mtu aliyechora ubavuni mwa nyumba ya mtu kwamba maisha ni binadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, hivyo aliwataka Skauti nao wawe hadithi nzuri kwa wale watakaosimuliwa habari zake.

Mwinyi alipewa nafasi ya kuzungumza baada ya Rais Magufuli kumuapisha katibu mkuu mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje, Faraji Mnyepe na Mahiza ambaye ni Skauti Mkuu.

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 15, Mwinyi alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo kuwataka viongozi wa Skauti wafanye kazi kwa kufuata kanuni ili wasimtie aibu yeye na Rais John Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya mdhamini wa Skauti nchini.

Mwinyi alianza hotuba yake kwa kuomba radhi, akisema ana tatizo lake la kusahau na kwamba hivi karibuni atatafuta mwalimu wa lugha ya Kiswahili kwa sababu kutokana na umri wake anasahau maneno mengi.

Alieleza namna anavyomhusudu Rais Magufuli kwa mambo makubwa ambayo anayafanya kwa maslahi ya Taifa. Alisema naye anatamani angekuwa kama Magufuli.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527