MO DEWJI AONEKANA HADHARANI KWA MARA YA KWANZAMo Dewji akiwa nje ya msikiti wa Shia, mtaa wa Idhira Gandhi jijini Dar es Salaam (picha kwa hisani ya Mwananchi) 

Bilionea Mo Dewji jana alisababisha mkusanyiko wa wananchi wenye shauku ya kumuona, baada ya gari lake lenye jina ‘Mo1’ kuonekana likiwa limepaki nje ya msikiti. 

Mo alihudhuria swala ya Ijumaa katika msikiti wa Shia, mtaa wa Idhira Gandhi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana hadharani tangu alipotekwa Oktoba 11 mwaka huu na kuachiwa huru baada ya siku tisa. 

Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, wananchi wengi pamoja na waandishi wa habari walilisogelea gari lake kwa lengo la kumuona. 

Umati huo ulimshuhudia Mo akiwa mtu wa mwisho kutoka msikitini pamoja na watu wake wa karibu, akiwa na walinzi pia. Alivalia mavazi meusi pamoja na miwani. 

Baada ya tendo hilo jema la kufanya ibada, Mo alifungua kioo na kutoa sadaka kwa baadhi ya watu waliolizunguka gari lake ambao hukaa karibu na maeneo ya mkusanyiko kuomba misaada. Bilionea huyo ambaye anamiliki karibu nusu ya hisa za Klabu ya Simba, alitekwa na watu wasiojulikana katika hotel ya Colosseum iliyoko Oysterbay jijini Dar es Salaam, alipoenda kufanya mazoezi alfajiri. 

Watesi wake walimtekeleza siku tisa baadaye katika eneo la Gymkhana, Posta jijini humo lakini hawakumdhuru. 

Kwa mujibu wa jeshi la polisi, watekaji hao walifanya tukio hilo kwa lengo la kujipatia fedha lakini walishindwa kufanikisha lengo lao na kwamba baada ya kuona wamekaribiwa na jeshi hilo waliamua kumtelekeza Mo na wao kutokomea kusikojulikana. 

Polisi walibaini gari aina ya Surf lililokuwa na watekaji ambao wametajwa kuwa ni raia wa kigeni, gari ambalo lilikutwa pia katika eneo la Gymkhana likiwa na silaha nzito za kivita.
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post