UTOUH: MSITUMIE MADARAKA KAMA MNAONGOZA FAMILIA ZENU

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema iko haja kwa wenye mamlaka kutengeneza nafasi zao zibaki kama taasisi na si kuzifanya kama mali ya familia.

Utouh alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye warsha ya asasi za kiraia (Azaki), ambako yeye na spika mstaafu, Anne Makinda walikuwa wasemaji kuhusu masuala ya uongozi.

Alisema kuna baadhi ya watu wameshindwa kutafsiri kuhusu dhana ya uongozi na badala yake wanachukua madaraka yanakuwa mali ya familia badala ya taasisi.

“Uongozi ni taasisi, tuepuke kufanya uongozi kuwa mali ya familia, hata kwenye urais msiruhusu aje mtu kufanya iwe ni mali ya familia wakati mnajua ni taasisi,” alisema Utouh ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Wajibu.


Utouh alisema uongozi siku zote ni jalala hivyo lazima pawepo na kuvumiliana ili kukubaliana kwa masilahi ya nchi.


“Kingine msifanye kazi kwa mazoea, yaani mtu anaingia na kudumu miaka mitano yote hakuna anachofanya badala yake ni kuendeleza waliyofanya wenzake tu, kwa nini usiwaze yako na wewe? Halafu lazima mfanye uamuzi siyo mtu analetewa faili anadumu nalo hata hafanyi uamuzi mwisho anachelewesha mambo,” alisema.
Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527