MO DEWJI ATAFUTWA MPAKA BAHARINI


Gari la Polisi likifanya doria katika maeneo ya fukwe za Yacht Club jijini Dar es Salaam jana. 

. Jeshi la Polisi Tanzania limeendelea kuimarisha ulinzi huku likifanya uchunguzi katika Pwani ya Bahari ya Hindi hususani katika hoteli zilizo ukanda huo ikiwamo Yacht Club.

Polisi hao wamekuwa wakikagua kamera za video (CCTV) katika hoteli ya Yacht Club, lengo likiwa ni kumsaka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliyetekwa juzi alfajiri na watu wasiojulikana.

Mo (43), alitekwa katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam saa 11 alfajiri alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye gym ya hoteli hiyo.

Meneja Mkuu wa Yacht Club, Brian Fernandez aliliambia Mwananchi jana kuwa tangu tukio la kupotea kwa Mo lilipotokea, polisi wameimarisha ulinzi na uchunguzi katika eneo hilo ambalo liko pwani ya Bahari ya Hindi.

Fernandez alisema Mo alikuwa mwanachama wa klabu hiyo na hakuonekana katika eneo hilo tangu juzi na hakuna boti ya mwanachama yeyote iliyoondoka tangu jana.

“Kama mwanachama anataka kwenda kwenye boti yake tunampeleka na boti yetu. Kwanza anaandika muda wa kuondoka na kurudi ili kama akichelewa afuatiliwe,” alisema.

Alisema Mo ni mtu maarufu na kama angefika eneo hilo angejulikana.

Awali, waandishi walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo maeneo ya Laibon, Oysterbay lakini walinzi waliwaambia msemaji wa familia amezuiwa kuzungumza na wanahabari.


Via>> Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post