KANGI LUGOLA : TUNAENDELEA KUMTAFUTA MO DEWJI...MPAKA SASA TUNASHIKILIA WATU 20


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema bado Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumpata Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliyetekwa siku tatu zilizopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Lugola alisema mpaka sasa kuna watuhumiwa 20 wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

"Na waliohusika na tukio hilo watasakwa mpaka pale watakapopatikana, tunavyozungumza sasa (saa 9 jioni), takribani watu 20 wanashikiliwa na kuhojiwa na Polisi, " alisema.

Hata hivyo, Lugola alisema watuhumiwa ambao hawaonekana hawakuhusika na tukio hilo wataachiliwa huru kabla ya saa 24, jambo ambalo pia alisema halijatekelezwa.

Waziri huyo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wote waliotekwa na kupotea hadi wapatikane.

"Kwa hiyo siyo kwamba limetokea tukio la MO Dewji ndio polisi wanafuatilia hilo tu. Polisi hawataacha kuwatafuta na kuwakamata na wengine waliohusika kwenye matukio mengine ili kuhakikisha wanapatikana," alisema.

Alisema kuna watu wanadhani polisi inaona MO Dewji ndiyo wa muhimu kumtafuta kuliko watu wengine jambo ambalo siyo sahihi.

"Ondoeni hiyo perception (dhana) kila Mtanzania anayo thamani sawa na mwingine," alisema.

Alisema Rais Magufuli ameapa kulinda uhai wa kila Mtanzania na mali zao, huku akiwataka waandishi wa habari kutoinyooshea kidole Serikali kwa utekaji huo..
Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post