BASI LA ARUSHA EXPRESS LAUA WATU WANNE

Watu wanne wamefariki dunia na wengine 10 wamejeruhiwa, baada ya basi la Arusha Express lililokuwa linatoka Arusha kwenda Mbeya kupata ajali na kupinduka eneo la Mlima Haraa Bonga mjini Babati mkoani Manyara.

Kamanda wa polisi mkoani Manyara, Agostino Senga amesema ajali hiyo imetokea leo Oktoba 8, 2018 saa 3:15 asubuhi wakati basi hilo lilipokuwa linapanda mlima.

Kamanda Senga amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo ila inaonyesha dereva alishindwa kukata kona kwenye mlima huo wa Haraa kisha gari likapinduka.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni kondakta wa basi hilo, Nasibu Ramadhani (43), Lawrence Mwajabara (46) mkazi wa Mbeya, Salvathory Thomas mkazi wa Bonga Babati na Jenny Mushi (21) mwanafunzi wa Bonga mjini Babati.

"Abiria watatu walifariki duniani papo hapo na mwingine mmoja alifariki dunia wakati anapelekwa hospitali kupatiwa matibabu," amesema Kamanda Senga.

Amesema majeruhi wa ajali hiyo ni 10 ambapo watano hali zao siyo nzuri na wengine watano wanaendelea vizuri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527