ASILIMIA 11 YA WATANZANIA KUWA WAZEE IFIKAPO 2050


Kamishna wa Ustawi wa Jamii Nchini Dkt. Naftali Ng’ondi akielezea lengo la kongamano kwa wazee waliohudhuria kongamano la wazee kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wazee yatakayofanyika Jijini Arusha Oktoba Mosi.
Mwenyekiti wa Kongomano la Wazee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wazee Tanzania Mzee Sebastian Bulegi akiongoza Wazee walioshiriki katika kongomano la wazee kwa lengo la kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wazee nchini wakati wa kongamano la wazee kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wazee yatakayofanyika Jijini Arusha Oktoba Mosi.
Mratibu wa huduma za Afya kwa Wazee kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Edward Mung’ong’o akiwasilisha mada wakati wa kongomano kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee leo Jijini Arusha.
Kamishana wa Polisi akieleze kuhusu hali ya mauaji ya wazee nchini na hatua zinazochukuliwa na jeshi hilo katika kupambana na vitebdo vya ukatili kwa wazee wakati wa kongomano kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee leo Jijini Arusha.

Wazee walioshiriki Kongamano la Wazee wakifuatilia mada mbalimbali zinazotolewa katika Kongamano hilo ikiwa ni moja ya shighuli zinazofanyika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yatakayofanyika Jiji la Arusha Oktoba Mosi. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

*** 
Tanzania inakadiliwa itakuwa na wazee 11% ya watu wote nchini ifikapo mwaka 2050, kwa kuwa idadi ya watu inaongezeka kwa kasi kutokana na kuendelea kuboreka kwa huduma za Afya hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Huduma za Afya kwa Wazee kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Edward Mung’ong’o wakati akiwasilisha mada kwenye kongomano lililofanyika leo Jijini Arusha kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee, amesema kuwa Mwaka 2002 idadi ya Wazee ilikuwa milioni 1.4, ikiwa ni sawa na 4% ya watu wote yaani Milioni 33.5. 

Aidha Dkt. Mung’ong’o amesema kuwa kwa sasa idadi ya Wazee hapa nchini inakisiwa kuwa milioni 3 sawa na 5.6% ya watu wote ambao kwa takwimu za sasa Tanzania ina Watu milioni 55.

Akizungumzia mafanikio ya serikali katika kuboresha huduma za Afya kwa Wazee Dkt. Mung’ong’o amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International imepitia na kuboresha Mtaala wa kufundishia Wauguzi ngazi ya kata ili wapate mafunzo yatakayowawezesha kuhudumia Wazee kwa ufanisi.

Aidha Dkt. Mung’ong,o aliongeza kuwa kwa kushirikiana na HelpAge International pia serikali imeandaa Mwongozo kwa ajili ya watoa huduma wa kuwaelekeza jinsi ya kutibu magonjwa ya kawaida yanayowasibu Wazee.

Wakati huo huo Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Naftali Ng’ondi akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alisema Wazee watatumia fursa hiyo kujadiliana juu ya utekelezaji wa Sera na Miongozo ya kuboresha hali na Maisha ya Wazee nchini kwa kuzingatia utambuzi wa wazee katika Halmashauri, upatikanaji wa huduma za Afya kwa wazee na ushirikishwaji wa wazee.

Aidha Kamishna Ng’ondi aliwaeleza wajumbe wa Kongamano hilo kuwa mengine yatakayojadiliwa ni Huduma za Afya kwa wazee na utekelezaji wa Mpango wa huduma Rafiki wa Afya kwa Wazee na mabadiliko ya Utaratibu wa Uchangiaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na azma ya Serikali Kufikia Pensheni ya Jamii kwa Wazee wote.

Aidha Dkt. Ng’ondi alisema kimsingi kongamano la Wazee pia litaangalia Sera na Mfumo wa Kodi unavyozingatia mahitaji ya makundi Maalumu Msamaha kwa Wazee hali ya Mauaji ya Wazee nchini na Jitihada za Kukabiliana na Hali hiyo.

Kamishna Ng’ondi alisema kuwa pamoja na umri mkubwa walionao wazee wana haki ya kuheshimiwa utu wao na kupata haki zote wanazostahiki kama binadamu ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kupata matunzo katika familia na kulindwa dhidi ya madhara yoyote yanayoweza kuwaathiri kimwili, kiakili, kihisia na kisaikolojia.

Wazee wamekutana leo Jijini Arusha kushiriki kongamano la Wazee katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayofanyika kitaifa Jijini Arusha kwa lengo kutoa fursa kwa wazee kujumuika kwa pamoja na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kuboresha hali ya maisha yao nchini

Siku ya Kimataifa ya Wazee huadhimishwa kufuatia Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 45/106 la mwaka 1990 linalozitaka nchi wanachama kutenga siku maalumu ya kutafakari mchango wa Wazee katika maendeleo ya jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527