WANANCHI WAFURAHIA HUDUMA BORA ZA AFYA KITUO CHA AFYA NYAKANAZI..RC GAGUTI ASHUHUDIA


Brigedia Jenerali Marco Gaguti ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kagera akitoa hongera kwa Scola Elias baada ya kujifungua katika kituo cha Afya Nyakanazi Wilayani Biharamulo ambapo amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Afya pamoja na kujitambulisha.Picha na Angela Sebastian  - Malunde1 blog
 ***
Wananchi wa kata ya Nyakanazi wilayani Biharamulo wamemueleza mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti kuwa wameanza kunufaika na huduma za Afya zinazotolewa katika kituo cha Afya cha Nyakanazi.

Manufaa hayo yameibuka baada ya Serikali kutoa Shilingi milioni 500 za kuboresha na kukarabati Kituo hicho kinachotoa huduma za afya kwa wananchi 19,172 ambapo uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wameweza kujenga majengo mapya na kukarabati ya zamani.

Ushuhuda huo ulitolewa na akina mama wazazi katika wodi ya wazazi kituoni hapo mara baada ya Brigedia Jenerali Gaguti kufika kituoni hapo jana na kutembelea na kukagua ubora wa majengo yaliyojengwa lakini pia kuangalia thamani ya fedha za Serikali kama inalingana na ujenzi huo. 

Kwa niaba ya akina mama wazazi waliokuwa wamepumzishwa katika wodi ya wazazi mara baada ya kujifungua watoto, Schola Elias (30) alimweleza Mkuu wa Mkoa Gaguti kuwa wanafurahia huduma za kituo hicho kwa kuboreka baada ya Serikali ya kuleta fedha za kujenga majengo mapya hasa chumba cha kujifungulia akina mama wajawazito na wodi ya wazazi pia na ukarabati majengo ya zamani.

“Kipindi cha nyuma chumba cha kujifungulia kilikuwa na vitanda vya wazazi viwili tu jambo liloleta usumbufu mkubwa sana lakini baada ya ujenzi mpya kuna vitanda vitano jambo ambalo linapelekea hata sisi akina mama wajawazito watano tunaweza kujifungua kwa wakati mmoja",alieleza Scola.

Alisema wodi ya zamani ilikuwa ina vitanda vinane tu lakini sasa kama kuna vitanda 25 vya kupumzikia baada ya kujifungua hivyo kwa sasa hakuna mama anakosa kitanda.

Naye afisa Muuguzi msaidizi Pili Ndamulo ambaye ni msimamizi wa wodi ya wazazi katika Kituo hicho alisema kuwa, wastani kwa wiki wanajifungua akina mama 30 hadi 40 na kwa mwezi ni akina mama 100 hadi 120.

Naye Mkuu wa Mkoa Gaguti akiongea na wananchi katika Kituo cha Nyakanazi mara baada ya kukikagua aliwataka wananchi hao kukitunza kituo hicho.

Pia aliwataka watumishi kutoa huduma zinazoendana na ubora wa majengo ya Kituo, wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa EBORA kwani Nyakanazi inazo njia kuu mbili zinazoelekea nchi jirani za Burundi, Rwanda na Kongo DRC na kuwashauri wananchi wote kujiunga na bima ya afya kwa ajili ya matibabu yao.

Majengo yaliyojengwa katika Kituo cha Afya Nyakanazi ni pamoja na Wodi ya Watoto, Wodi ya Akina Mama Wazazi, Nyumba ya Watumishi wawili, Chumba cha kuhifdhia maiti, jengo la kujifungulia, Njia za kutembelea na Kichomea taka. 

Majengo yaliyokarabaitiwa ni pamoja na jengo la wagojwa wa nje, Jengo la upasuaji na Mahabara. Ujenzi huo umefanyika kwa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 566 fedha hizo zikijumuisha fedha za Serikali Kuu, Halmashauri ya Wilaya pamoja na mchango wa wananchi wa Nyakanazi.
Na Angela Sebastian - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post