Picha : MIGODI YA BUZWAGI NA BULYANHULU YALIPA MILIONI 771 KWA AJILI YA USHURU WA HUDUMA KAHAMA MJI NA MSALALA


Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Acacia kupitia migodi yake ya Buzwagi na Bulyahulu iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imekabidhi hundi zenye thamani ya shilingi milioni 771 kwa halmashauri ya Kahama Mji na Msalala.Akikabidhi hundi za fedha hizo leo Septemba 13,2018 kwenye ofisi za mkuu wa wilaya ya Kahama, Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu amesema katika fedha hizo Milioni 771 zimegawanywa mara mbili, ambapo mgodi wa Buzwagi umeilipa halmashauri ya Kahama mji ushuru wa huduma shilingi 650,479,914.38.

Amesema katika Mgodi wa Bulyanhulu umeilipa halmashauri ya Msalala ushuru wa huduma shilingi 121,349,478, na hivyo kufanya jumla ya fedha zote zilizotolewa na migodi hiyo miwili ambayo ipo chini ya Kampuni ya Acacia kuwa shilingi  771,829,392.

Alisema fedha hizo zimetolewa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi June 2018, ikiwa ni malipo ya mikataba ya makubaliano kati ya migodi hiyo miwili na halmashauri husika kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma katika jamii zinazozunguka migodi ikiwamo sekta ya afya, elimu pamoja na maji salama.

“Natoa rai kwa halmashauri hizi mbili ambazo zimepokea hundi leo kuzitumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hasa wanaozunguka migodi hii miwili ya Buzwagi na Bulyanhulu,”alisema Busunzu.

“Licha ya migodi hii kulipa kodi stahiki, bado imekuwa ikijishughulisha katika kuhakikisha ina kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali katika maeneo yanayotuzunguka, tukiwa na lengo la kuinua uchumi wa wilaya pamoja na kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi,”aliongeza.


Aidha alisema wanajivunia kuwa wadau muhimu wa maendeleo kwa halmashauri na taifa kwa ujumla, na kuipongeza serikali kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiuonesha katika utekelezaji wa miradi yao, ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga jamii endelevu, na hatimaye kuendana na mpango endelevu wa miaka mitano na dira ya taifa ifikapo 2025.

Naye mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha aliipongeza migodi hiyo kwa kutoa hundi hizo na kutoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili Msalala na Kahama Mji kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo kulipana posho na semina.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa Kahama Mji Clemence Mkusa alisema baadhi ya fedha hizo watazielekeza kwenye ukarabati wa majengo katika hospitali ya wilaya ya Kahama ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Nae Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala Dk. Ntanwa Kilagwile, alisema baadhi ya fedha hizo wao watazielekeza kwenye ukarabati wa vyumba vya madarasa pamoja na matengezo ya magari na kuahidi kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Migodi hiyo ya Buzwagi na Bulyanhulu ambayo ipo chini ya Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu (ACACIA), hulipa ushuru wa huduma hizo kwenye halmashauri zinazowazunguka kila baada ya miezi sita.

Tangu kuanzishwa kwa mgodi wa Buzwagi mwaka (2009-2017) wameshalipa ushuru wa huduma shilingi Bilioni 5.5 ambapo Mgodi wa Bulyanhulu tangu mwaka (2000 -2017 umeshalipa Shilingi Bilioni 13.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Kushoto ni Meneja mkuu wa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu akikabidhi hundi ya ushuru wa huduma shilingi  650,479,914.38 kwa halmashauri ya Kahama Mji, Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akifuatiwa na Kaimu mkurugenzi wa Kahama mji Clemensi Mkusa.

Meneja mkuu wa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu akishikana mkono wa pongezi na kaimu mkurugenzi wa Kahama Mji Clemence Mkusa, katikati ni mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha.
Meneja mkuu wa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu akishikana mkono wa pongezi na kaimu mkurugenzi wa Msalala Dkt Ntanwa Kilagwile wakati akikabidhiwa hundi ya ushuru wa huduma shilingi 121,349,478, katikati ni mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha.Wa kwanza kushoto ni Meneja mkuu wa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi Benedict Busunzu akikabidhi hundi ya ushuru wa huduma shilingi 121,349,478 kwa halmashauri ya Msalala, Katikati ni mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akifuatiwa na Kaimu mkurugenzi wa Msalala Dkt. Ntanwa Kilagwile.

Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akimkabidhi Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji Clemensi Mkusa hundi ya ushuru wa huduma kutoka mgodi wa Buzwagi 

Meneja mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akizungumza mara baada ya kumaliza kukabidhi hundi ya ushuru wa huduma Milioni 771 kwa halmashauri ya Kahama Mji na Msalala na kutaka fedha hizo zikatumiwe kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wanaoizunguka migodi hiyo miwili.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akizungumza mara baada ya kumaliza kupokea hundi ya ushuru wa huduma kutoka kwenye migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu. Aliagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili Kahama Mji na Msalala kuwa fedha hizo zisitumike kwa kupeana posho wala semina.

Kaimu mkurugenzi wa Kahama Mji Clemence Mkusa, akizungumza baada ya kumaliza kupokea hundi ya ushuru wa huduma kutoka katika Mgodi wa Buzwagi Shilingi 650,479,914.38 .

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala Dkt Ntanwa Kilagwile, akizungumza baada ya kumaliza kupokea hudi ya ushuru wa huduma kutoka mgodi wa Bulyanhulu Shilingi 121,349,478.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Aamringi Macha akizungumza baada yakupokea hundi hizo.

Awali Meneja mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhuru Benedict Busunzu akizungumza na vyombo vya habari kabla ya kuanza zoezi la kutoa hudi za ushuru wa huduma kwenye halmashauri za Kahama Mji na Msalala.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akiteta jambo na Meneja mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu baada ya hafla fupi kumaliza kulipa ushuru wa huduma katika halmashauri ya Kahama Mji na Msalala.

Meneja mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu wa kwanza mkono wa kushoto akishikana mikono ya pongezi na Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji Clemensi Mkusa, baada ya kumalizika kwa zoezi la utolewaji wa hundi za ushuru wa huduma.

Viongozi wa Serikali wilayani Kahama wakipiga picha ya pamoja na meneja mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu baada ya kumalizika kwa zoezi la utolewaji wa hudi za ushuru wa huduma kwenye halmashauri ya Kahama Mji na Msalala.

Na Marco Maduhu- Malunde1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post