RC GAGUTI AAHIDI KUSHUGHULIKIA HARAKA MGOGORO WA ARDHI KATI YA WAKULIMA NA WAWEKEZAJI VITALU VYA NARCO


Kulia ni Meneja wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mkoani Kagera Mashaka Mlonge akitoa maelezo kwa mkuu wa Brigedia jenerali Marco Gaguti kuwa NARCO sasa inafanya tathmini upya kuona wawekezaji ambao hawajawekeza na kuviendeleza vitalu vyao kama walivyokubaliana na Serikali ambapo tayari Vitalu vitano kati ya 54 vilivyopo mkoani Kagera Wawekezaji wake wamepewa “notice” ya kuachia vitalu hivyo. Picha na Angela Sebastian - Malunde1 blog
**

Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco  Gaguti amewaahidi wananchi wa Rutoro wilayani Muleba ambao ni wakulima kuwa atashughulikia haraka migogoro ya ardhi kati yao na Wawekezaji wenye vitalu katika Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mkoani Kagera ili wawekezaji waweze kufuga kwa tija na wakulima waendeshe kilimo chao bila kuingiliana na wawekezaji ambao ni wafugaji.

Mkuu wa Mkoa Gaguti ametoa ahadi hiyo wakati akitembelea vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Kikurula Wilayani Karagwe na Kagoma Wilayani Muleba ambapo alikagua uwekezaji wa NARCO eneo la Kikurula na kukutana na wananchi wa Rutoro ambao wana mgogoro wa muda mrefu na wawekezaji ambao walipewa vitalu na Serikali kuendesha ufugaji wa kisasa na baadhi ya vitalu hivyo kuvamiwa na wananchi hao.

Wakitoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Wananchi wa Rutoro  walidai kuwa wanashindwa kuendeleza maeneo yao ya kilimo kutokana na Serikali kutomaliza mgogogro kati yao na Wawekezaji ambao ni wafugaji na mgogoro huo umedumu kwa takribani miaka kumi na miwili toka mwaka 2006 hadi sasa.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo kutoka kwa wananchi na kutembelea Vitalu vya wawekezaji ambao ni wafugaji Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaeleza wananchi wa Rutoro pamoja na Wawekezaji kuwa alikwenda maeneo hayo kujifunza, kuona na kusikia mwenyewe juu ya mgogoro huo ili autafutie ufumbuzi wa haraka ili kila upande uendelee na shughuli zake za kulijenga taifa.

Katika hatua nyingine Meneja wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mkoani Kagera Mashaka Mlonge alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa NARCO sasa inafanya tathimini upya kuona wawekezaji ambao hawajawekeza na kuviendeleza vitalu vyao kama walivyokubaliana na Serikali ambapo tayari Vitalu vitano kati ya 54 vilivyopo Mkoani Kagera Wawekezaji wake wamepewa “notice” ya kuachia vitalu hivyo.

Na Angela Sebastian - Malunde1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527