RAIS MAGUFULI ATANGAZA MAOMBOLEZO YA KITAIFA SIKU NNE ...ALIYEKUWA ANAENDESHA MV NYERERE NI 'DEIWAKA'

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kuhusiana na ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari zake  kati ya kisiwa cha  Bugolora na Ukara katika ziwa Victoria  Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza ambapo  watu 131 wanahofiwa kupoteza maisha. Pia Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku nne za Maombolezo kuanzia leo tarehe 21 Septemba 2018. 
Rais John Magufuli amehutubia waandishi muda mfupi uliopita na ameeleza kuwa kufikia sasa imethibitika kwamba miili ya watu 131 imeopolewa na bado kuna hofu kwamba wengine wengi hawajapatikana.

Ameeleza kuwa rasmi kivuko hicho cha MV Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kwa takwimu zilizopo sasa zinazojumuisha miili iliyopatikana pamoja na manusura, ni wazi kwamba chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria kupita kiasi.

Rais Magufuli ameagiza bendera ya taifa ipepee nusu mlingoti na kutangaza maombolezo ya kitaifa siku nne kuanzia leo.

. Rais Magufuli amedokeza mambo yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo kuwa ni pamoja na nahodha wa kivuko hicho kuwa si mwenyewe ila ‘deiwaka’.

Amesema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu 100 au 101 lakini ilibeba watu zaidi, “Taarifa za awali, tulizopata kutoka kwa mashuhuda, Kivuko hicho mpaka sasa hivi (saa 1.14 jioni) maiti 131 na majeruhi 40, tayari imefika 171 na maiti bado wako.”

“Hata aliyekuwa anaendesha hiyo feri, siyo nahodha mwenyewe, yeye hakusafiri na inadaiwa amekamatwa na wote wakamatwe,” amesema huku akisisitiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote waliohusika.

Katika hotuba yake ya chini ya dakika kumi, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kutokutumia msiba huo kisiasa, “Tuviache vyombo vinavyohusika na uchunguzi, vifanye kazi yake, vifanye uchunguzi vitatoa taarifa.”

“Wale watakaobainika watafikishwa mahakamani na vifo vya Watanzania tusivitumie kisiasa, vyombo vyenye utaalamu vitatoa taarifa yake,” ameongeza:

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527