MWANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE MBARONI KWA KUTUPA MTOTO CHOONI


 KUTUPA MTOTO – JIJINI MBEYA
JESHIi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja ambaye amefahamika kwa jina la INES MTUNDU [19] Mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Isengo kwa kosa la kumtupa chooni mtoto mchanga wa masaa kadhaa. 

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 23.09.2018 majira ya saa 09:53 asubuhi huko maeneo ya Isengo – Airport ya zamani, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mjamzito na mara baada ya kujifungua chooni ndipo alimtupa mtoto huyo. 

Mara baada ya taarifa kulifikia Jeshi la Polisi, jitihada za haraka zilifanyika kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na kufanikiwa kumuokoa mtoto huyo akiwa hai. Mama na mtoto huyo wote wapo Hospitali ya Wazazi – Meta wakipatiwa matibabu. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani. 

KUPATIKANA NA BHANGI – KYELA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la GOLIATH EMANUEL [43] Mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi debe sita nyumbani kwake. 

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 22.09.2018 majira ya saa 23:47 usiku huko Kasumulu, Kata ya Ngana, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela katika msako uliofanyika maeneo hayo. Mtuhumiwa alikuwa ameificha bhangi hiyo katika mifuko ya salfeti nyumbani kwake. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani. 

MAUAJI – CHUNYA
Mnamo tarehe 22.09.2018 majira ya saa 15:00 alasiri huko katika kitongoji cha kasisi, kijiji cha nkwangu, kata ya upendo, tarafa ya kipembawe, wilaya ya chunya, mtu mmoja aitwaye LUTONJA LUKELESHA [33] Mkazi wa Kasisi alifariki dunia akiwa anajipatia matibabu kienyeji nyumbani kwake. 

Inadaiwa kuwa marehemu alipigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kukanyagwa kwa miguu kifuani na tumboni siku ya tarehe 12.09.2018 majira ya saa 12:09 mchana huko kijiji cha Kasisi na kaka yake aitwaye MASANILA LUKELESHA [45] Mkazi wa Kasisi akiwa na wenzake wawili. 

Chanzo cha tukio hili ni tuhuma za wizi wa radio ndogo yenye thamani ya Tshs 15,000/= ya mmalila mchoma mkaa ambaye jina lake halisi bado kufahamika. Mtuhumiwa mmoja MASANILA LUKELESHA amekamatwa na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili waliokimbia unaendelea. 

Katika kudhibiti ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na doria katika maeneo ya mlima nyoka [barabara kuu ya Mbeya-Njombe-Iringa], mlima iwambi [barabara kuu ya Mbeya – Tunduma], mlima Igawilo [barabara kuu ya Mbeya – Tukuyu] na Kawetele [barabara kuu ya Mbeya – Chunya]. Aidha katika operesheni ya kukamata bajaji zinazokiuka sheria za usalama barabarani ndani ya Jiji la Mbeya kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2018 jumla ya bajaji 170 zimekamatwa, madereva 31 wamefikishwa Mahakamani na bajaji 91 zimelipa tozo sawa na Tshs.2,730,000/= na bajaji 75 bado zipo kituoni kwa hatua zaidi za kisheria na watuhumiwa 14 wapo rumandewakiendelea na mashauri yao. 

Imesainiwa na: 
[ULRICH O. MATEI - SACP] 
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527