MKOA WA KIGOMA WAZINDUA KAMPENI YA FURAHA YANGU


Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga amewataka wanaume mkoani Kigoma kujitokeza kwa wingi kupima VVU na kufahamu hali zao ili wanapogundulika na VVU waweze kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU mara wanapogundulika na maambukizi.

Maganga ameyasema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa kampeni iliyozinduliwa kimkoa Wilayani Uvinza katika Tarafa ya Nguruka ya kuhamasisha wananchi hususan wanaume kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema.

Maganga amewasihi wanaume kuacha tabia ya kumsindikiza mama kwamba akipima yeye pekee basi nao wanadhani wapo sawa.

Akielezea madhumuni ya kampeni hiyo, kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Hosea amesema Kampeni hiyo ya kitaifa yenye kauli mbiu “Furaha Yangu – Pima, Jitambue, Ishi”. Inaweka mkazo na kuhamasisha zaidi wanaume kupima ili kutambua hali zao za maambukizo ya VVU. 

Alisema  mpango huo una lengo la kumwanzishia dawa za ARVs kila mtu aliye na maambukizi ya VVU ili aweze kuishi maisha ya furaha bila kuwa na hofu ya kupata magonjwa nyemelezi.

Aidha amezitaka Halmashauri Mkoani humo kwa kushirikiana na wadau wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kufanya kampeni ya upimaji kwa wanaume mfululizo ili hadi mwezi Desemba mwaka huu 2018 wakati wa Maadhimisho ya siku ya UKIMWI, kuweza kupata hali halisi ya maambukizi katika mkoa wa Kigoma.

"Wakuu wa Wilaya kwa kusaidiana na Wakurugenzi wa Halmashauri simamieni kampeni hii kwa uzito unaostahili, pia anzisheni mpango wa kuendesha upimaji kila panapokuwepo mikusanyiko katika Wilaya zenu” ,amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Alisema ili kuendelea kupambana na maambukizi mkoani Kigoma Halmashauri na Idara ya Afya zimeshauriwa kuhakikisha zinawatumia vyema Watu wanaoishi na VVU (WAVIU), hasa waliojiweka wazi hali zao, kuwahamasisha watu wanaorudi nyuma katika matumizi ya dawa za kufubaza (ARV) nchini Tanzania

Hamasa miongoni mwa wananchi na hasa wanaume katika kuziendea huduma za upimaji wa VVU nchini bado ni ya kiwango cha chini Matokeo ya awali ya Utafiti uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia mwezi Oktoba 2016 hadi Agosti 2017, yanaonesha ni asilimia 52.2 tu ya wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 – 64 walitoa taarifa kuwa wanajua hali zao za maambukizo ya VVU, (Wanawake ni asilimia 55.9 na Wanaume ni asilimia 45.3) WAVIU wa umri wa miakan 15-64 walitoa taarifa ya hali zao.

Editha Karlo-Malunde1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emanuel Maganga akiwaongoza wananchi kupima VVU katika kampeni ya uhamasishaji kwa wanaume kupima VVU
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwamvua Mrindoko akishiriki kupima VVU katika uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu Mkoani Kigoma





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527