MBUNGE WA CHADEMA ATEMBEZEWA KICHAPO NJE YA KITUO CHA POLISI


Mbunge wa Rombo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Selasini, amedai kuvamiwa na kupigwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Kenani Kihongosi nje ya Kituo Kidogo cha Polisi cha Mto wa Mbu mjini hapa.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu, mbunge huyo alidai kupigwa na mwenyekiti huyo, huku akishuhudiwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa CCM, Mariam Ditopile.

Alidai tukio hilo lilitokea saa 4 asubuhi wakati alipokwenda kituoni hapo kuwadhamini vijana wao wa Chadema waliokuwa wamekamatwa na watu aliodai kuwa ni kikosi cha ulinzi cha CCM maarufu kama Green Guard saa tano usiku wa kuamkia jana na kuwaweka chini ya ulinzi hadi saa 10 alfajiri na kisha kuwapeleka polisi.

Selasini alisema akiwa nje ya kituo hicho, baada ya mazungumzo na mkuu wake, ghafla lilifika gari aina ya Land Cruiser linalotumika kubeba watalii likiwa na kundi la vijana, miongoni mwao wakiwamo Kihongosi na Mariam.

Alisema pamoja na mambo mengine aliyoyakuta kituoni hapo na gari hilo lilimshtua na hivyo kuamua kuchukua simu yake kupiga picha, kitendo ambacho kiliwafanya vijana waliokuwamo katika gari hilo kushuka na kuhoji.

“Nilikuwa napiga picha ili baadae tuje tuitumie kama ushahidi, ile nachukua picha tu ghafla vijana hao wakashuka na kuhoji kwanini nawapiga picha, nikawaambia kwamba tukio hilo ni ‘public’ mbona rais akiwa ziara anapigwa picha, wakaanza kunipiga, nikawaambia kama nimekosea basi mnisamehe, lakini bado waliendelea kunipiga.

“Na aliyenipiga sana ni huyu Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, huku Mariam Ditopile akiwa anashuhudia, nikamuuliza Mariam wewe ni mbunge mwenzangu mbona hunisaidii, yeye ananiangalia tu na kucheka,” alisema Selasini.

Alisema kipigo hicho kimemsababishia maumivu makali ikiwa ni pamoja na kuvimba usoni na hivyo kulazimika kunywa dawa za kutuliza maumivu na kisha kujikanda kwa barafu.

Alidai kuwa baada ya kumpiga, vijana hao walimnyang’anya simu yake ambayo alisema amepata taarifa waliipeleka katika kituo hicho cha polisi.

Alisema Mkuu wa Kituo hicho baadae alitoka nje na kukuta purukushani na kwa busara alimaliza mgogoro uliokuwapo.

Gazeti hili jana lilimtafuta Mariam kwa njia ya simu ambaye baada ya kusikiliza sababu za kupigiwa simu alimwambia mwandishi ampigie baada ya nusu saa.

Alipotafutwa baada ya nusu saa hakupokea simu tena.

MTANZANIA Jumapili jana liliwasiliana na Mwenyekiti wa UVCCM Iringa, Kihongosi ambaye alisema hayupo Monduli na wala hajakanyaga katika kipindi chote cha kampeni.

“Hapa natokea Ihemi kwenye kambi ya vijana ambako nilikuwa tangu tarehe 10 mwezi huu, sasa hivi nipo Mufindi hapa naangalia mpira, unasikia makelele hayo,” alisema Kihongosi.

Alisema Selasini amemsingizia na amemuonea na hajui agenda yake ni nini hasa.

“Mimi naona ni kuchanganyikiwa kisiasa, nawashauri wafanye siasa safi,” alisema Kihongosi.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi, alisema amesikia malamiko hayo ya Selasini yakizungumzwa kwenye majukwaa.

Ng’anzi alimshauri Selasini kwenda Kituo cha Polisi Mto wa Mbu akatoe taarifa ili kuwezesha hao waliofanya kitendo hicho kukamatwa.

Awali akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea, Mwenyekiti wa wa taifa wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi, alidai mbunge huyo alivamiwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali ikiwamo usoni, kunyang’anywa simu na kuvunjiwa miwani.

Akizungumzia mwenendo wa kampeni hizo, Ole Sosopi alilalamikia baadhi ya mawaziri kutumia magari ya Serikali kumpigia kampeni mgombea wa CCM, Julius Kalanga na kuahidi wananchi kuwapelekea huduma mbalimbali ikiwamo maji, umeme na kutatua migogoro ya ardhi.

Alidai kwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria za uchaguzi zinazokataza magari ya umma kutumika kufanya kampeni.

Sosopi alisema kutoa ahadi hizo wakati wa kampeni ni sawa na rushwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, walilazimika kuandika barua Tume ya Maadili ambayo mwenyekiti wake ni Msimamizi wa Uchaguzi na nakala kupeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lakini hadi sasa hawajajibiwa chochote wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

Sosopi alilaani vitendo vya vitisho dhidi ya baadhi ya mawakala wao hasa maeneo la Mto wa Mbu na Makuyuni.

Akijibu malalamiko hayo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Monduli, Steven Ulaya, alisema hajapokea barua yoyote ya malalamiko na kuwa kampeni zimeendeshwa na vyama vyote kwa amani na utulivu.

Na JANETH MUSHI -MONDULI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post