MKUU WA MAJESHI JENERALI VENANCE MABEYO ASEMA WATATUMIA SIKU 2 KUKINYANYUA KIVUKO CHA MV NYERERE

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema kivuko cha Mv Nyerere kitapinduliwa chini juu hapo kilipo badala ya kuvutwa hadi mwaloni kama mipango ya awali ilivyokuwa.


Jenerali Mabeyo ametoa kauli hiyo jana, Septemba 23, 2018 eneo la Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza baada ya kuwasili kifaa maalumu kitakachotumika kukipindua kivuko kilichozama Septemba 20,2018 na kusababisha vifo vya watu 224 hadi sasa.


“Tuombeni tufanikiwe na tutafanikiwa. Tunaamini kazi hii ya kukipindua kivuko hiki itaweza kuchukua siku mbili au tatu,”


“Kivuko hiki kimejikita chini na kifaa hiki kitaingiza upepo utakaoingia kwenye maboya yatakayosaidia kukipindua na hatua ya kukipindua itasaidia kivuko hiki kutoharibika,” alisema Jenerali Mabeyo.


Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema shughuli ya uokoaji inafanywa na Watanzania wenyewe na si watu kutoka nje.


Pia, amewapiga marufuku watendaji wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kukodi vifaa kwa ajili ya shughuli hiyo na kwamba kazi hiyo ipo chini ya uratibu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527